• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
UJAUZITO NA UZAZI: Kuvuja damu wakati wa ujauzito katu si dalili nzuri

UJAUZITO NA UZAZI: Kuvuja damu wakati wa ujauzito katu si dalili nzuri

Na PAULINE ONGAJI

KUNA baadhi ya wanawake wanaokanganyikiwa wakiwa wajawazito hasa wanapoanza kuvuja damu kutoka ukeni.

Kuna baadhi wanaodhani kwamba damu hiyo ni ya hedhi, lakini ukweli ni kwamba ukiwa mjamzito, haiwezekani kushuhudia hedhi.

Hii ni kwa sababu mzunguko wa kihomoni kila mwezi umekatizwa, na ukuta wa uterasi ambao huambuka kila mwezi wakati wa hedhi sasa unatumika kumkuza mtoto aliye tumboni.

Hata hivyo, unaweza vuja damu ukiwa mjamzito, wakati ambapo mimba inajitundika kwenye ukuta wa uterasi.

Damu hii hutoka wiki za awali za ujauzito na kwa kawaida haitoki kwa wingi.

Aidha, unaweza vuja damu kutokana na mwasho kwenye lango la uzazi, au ikiwa kuna maambukizi, au ikiwa mimba imejitundika nje ya uterasi (ectopic pregnancy), au ikiwa kuna hatari ya mimba kutoka.

Kwa kawaida matatizo haya huhitaji kuangaliwa na mwanajinakolojia. Aidha, huenda uchunguzi wa maabara ukahitajika na wakati mwingine kupigwa picha ya sehemu ya nyonga.

Ikiwa mimba yako imejitundika nje ya uterasi na unavuja damu, basi upasuaji wa dharura hufanywa. Ikiwa ni mimba inatoka, utalazwa hospitalini upokee matibabu.

Wakati mwingine, kuvuja damu hutokana na kuwa tayari mimba inatoka na hivyo huenda ukapewa dawa au ukafanyiwa utaratibu wa kimatibabu.

You can share this post!

Washambuliaji Dennis na Osimhen watupwa nje ya kikosi cha...

Wanaume watalimana leo Stamford Bridge

T L