• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
PAUKWA: Bahati amtapikia mamaye nyongo

PAUKWA: Bahati amtapikia mamaye nyongo

NA ENOCK NYARIKI

“KWA nini kila wakati baba hapendi kutimiza ahadi yake?’’ Bahati alimuuliza mama yake baina ya kilio cha kusinasina.

‘‘Mwanangu, baba yako aliitwa ghafla kazini ikambidi kufutilia mbali mpango wa kuja kukutembelea. Hata hivyo, kwa kuwa mimi mama yako nimefika…..”

“Nimechoka! Nimechoka kugeuzwa kinyago cha kuchekwa na wenzangu kwa sababu ya sura yako ya kutisha!’’ Bahati alimtapikia mama yake yote aliyokuwa nayo moyoni.

Maneno yale yalipita katika sikio la Cheusi kama upepo wenye sumu na kupiga fundo kwenye moyo wake. Kwa dakika kadhaa alisimama kimya bila kunena jambo ili kuyaruhusu maneno yenyewe kuteremka kimyakimya kwenye viungo vyake vya ndani.

Ghafla, machozi yalianza kumtiririka maskini mwanamke yule kama maji kwenye bilula. Mama na mwana walilia asiwepo wa kumfariji mwenzake.

Cheusi alikumbuka jinsi alivyohatarisha maisha yake ili kuyaokoa ya Bahati. Msimu ule wa kipupwe ulimkumbusha takribani misimu kumi na sita iliyopita. Wakati huo, Bahati alikuwa kitoto kidogo cha umri wa miezi tisa pekee.

Cheusi alikuwa kwenye kibanda chake cha kuuzia mboga kwenye mtaa wa mabanda wa Kisera. Kwa sababu ya baridi shadidi iliyoenea kote, biashara ilijikokota. Bi Cheusi alikuwa akimpimia mteja wake dagaa wakati tukio la kushtua lilipotokea. Mtoto wa jirani yake alifika kibandani huku pumzi za mjusi zikimwenda mbiombio

“Mama Bahati!….,’’ mtoto yule mwenye umri wa miaka tisa alitamka na kusita.

HADITHI ITAENDELEA

You can share this post!

TAHARIRI: Washambuliao wanahabari nao wakabiliwe

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu bora hufanya utafiti

T L