• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
PAUKWA: Bahili aokolewa na msamaria mwema

PAUKWA: Bahili aokolewa na msamaria mwema

NA ENOCK NYARIKI

POPO walipapatika na kulia kwa sauti msituni.

Chiriku alilia mfululizo kutoka sehemu fulani ya msitu. Ilikuwa asubuhi mbichi yenye baridi shadidi. Baridi ya mji mdogo wa Konabaridi ambayo ilimtafuna Bahili usiku kucha na kufanya vimbimbi kutuna kwenye ngozi. Miguuu ilikufa ganzi na mbavu kumuuma.

“Nilijipataje huku?” mzee yule ambaye alikuwa ameanza kurejelewa na fahamu alijiuliza.

Kutokana na maumivu makali ya mbavuni yaliyosababishwa na wahuni, asingeweza kutembea.

Ilimbidi atambae kutoka katikati ya msitu ili akatafute msaada. Kwa nyota ya jaha, aliviona vimulivumuli vya taa za magari kwa mbali.

Alijiburuta kwa bidii zaidi mpaka kandokando ya barabara ya lami ya Magadi-Kiserian. Mwanamume mmoja mmiliki wa gari la kibinafsi aliweza kukitambua kiwiliwili cha Bahili na kushika breki.

“Mzee, kuna shida gani?’’ alimwuliza Bahili ambaye sasa alionekana vizuri kwenye mwangaza wa gari.

“Wameniumiza na kuniibia kila kitu,’’ alisema kwa maumivu.

“Pole mzee! Mshukuru Mungu kwamba walikuibia kila kitu wakakuachia uhai. Twende ukatibiwe kwanza.’’

Msamaria mwema alikunja kiti cha nyuma cha gari na kumsaidia Bahili kujilaza garini. Gari lilipokuwa limeshika kasi kuelekea hospitalini kwenye mji wa Kiserian, Bahili alikuwa na ombi moja kwa mhisani wake:

“Mwanagu, usinipeleke kwenye hospitali ghali kwa sababu wameniibia pesa zote.”

‘‘Usijali mzee, nitalipa bili yote ya hospitali,” mwenye gari alisema baina ya kicheko cha mshangao.

Kweli mali ya bahili…

  • Tags

You can share this post!

TALANTA YANGU: Anainukia katika uchoraji vibonzo

Kilifi Ladies yaanza Ligi ya Kanda kwa kishindo

T L