• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
PCPB yaendelea kunyoosha mjeledi kwa wahuni wa dawa bandia za wadudu

PCPB yaendelea kunyoosha mjeledi kwa wahuni wa dawa bandia za wadudu

Na SAMMY WAWERU

BODI ya kutathmini na kudhibiti kemikali zinazotumika kukabiliana na wadudu shambani (PCPB) imetoa onyo kali kwa wahuni wenye mazoea kuunda na kutengeneza dawa bandia.

PCPB imesisitiza itaendelea kukamata wahusika na kuwachukulia hatua kali kisheria.Afisa Mkuu Mtendaji, Dkt Esther Kimani amesema bodi hiyo inafanya kazi kwa karibu na Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) kuwatia nguvuni.

Dkt Esther aidha alifichua taasisi hiyo ya serikali imepokea zaidi ya visa 10.“Tayari tumefikisha wahusika kortini, na wamefunguliwa mashtaka,” akaambia Taifa Leo.Alisisitiza kwamba PCPB haitalegeza kamba mikakati iliyoweka kukabiliana na dawa bandia na ghushi za wadudu.

“Lazima chakula kinachotufikia mezani kiwe salama,” Dkt Esther akasema. Afisa huyo alisema bodi yake ni makini katika kusajili na kuzipa kibali kampuni za kutengeneza dawa za wadudu.

Vilevile, alisema PCPB inaendeleza oparesheni kukagua maduka ya kuuza bidhaa za kilimo ili kubaini ikiwa dawa za wadudu zinazouzwa zimeafikia ubora wa bidhaa.

“Kwa wakulima, ninawashauri watumie dawa ambazo ni salama kwa mimea na mazao wanapokabiliana na kero ya wadudu,” akahimiza. Dkt Esther pia amewataka kukumbatia matumizi ya dawa asilia, ambazo hazijatengenezwa kwa kutumia kemikali.

Dkt Esther Kimani, Afisa Mkuu Mtendaji PCPB anasema bodi yake haitasaza wahuni wa kutengeneza na kuuza dawa ghushi na bandia za wadudu shambani….Picha/ SAMMY WAWERU.

Soko la kilimo na ufugaji, linaendelea kukumbwa na changamoto ya uuzaji wa bidhaa bandia na ghushi. PCPB inasema miongoni mwa mikakati na mipango yake kuboreshha huduma za dawa dhidi ya wadudu, inapania kuibuka na mfumo kutambua dawa halali na ambazo zimeafikia ubora wa bidhaa.

“Matumizi ya kodi mkulima anaponunua dawa na kukagua uhalisia wake yatatufaa pakubwa kupambana na wahuni,” akasema.

You can share this post!

MCA asikitishwa na wakulima kuendelea kuasi kahawa

Amepania makubwa katika tasnia ya uigizaji

T L