• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
PENZI LA KIJANJA: Ashiki ni kama pombe, ukilewa utajuta…

PENZI LA KIJANJA: Ashiki ni kama pombe, ukilewa utajuta…

NA BENSON MATHEKA

UNAHISI amekupagawisha hadi unakosa usingizi ukimuwaza?

Unashindwa kula au kufanya kazi ukimfikiria? Usipomuona au kuzungumza naye unajihisi mgonjwa?

Na licha ya haya yote anakuonyesha dharau, hivi kwamba kwake, ni kama hauko katika akili, moyo na mipango yake? Anakujali unavyomjali? Ikiwa la, basi unafaa kujanjaruka mapema. Penzi la aina hii, au likifikia hali hii linaweza kukutumbukiza pabaya. Na cha mno huenda si mapenzi ya dhati.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya mapenzi, ukweli mchungu ni kwamba mtu huwa ametekwa na kupumbazwa na penzi hewa.

“Zile hisia kali kuhusu mtu mwingine sio mapenzi hasa, ni ashiki tu. Zinafanya mtu kughururika, akawa anaona hawezi maisha bila anayemtamani. Mara nyingi huwa na nguvu na mtu anaweza kufanya jambo lisilo la kawaida kwa sababu ya ashiki,” asema Benard Mithika, mwanasaikolojia katika Shirika la Maisha Mema, Nairobi.

Mithika anasema ashiki huteka sana watu wa umri mdogo wanaoanza maisha ya mapenzi.

“Wengi wanaojipata katika hali hii wana umri wa miaka 19 na 30. Utafiti unaonyesha kuwa umri unavyozidi, ndivyo mtu anavyopungukiwa na ashiki,” asema.

Watu wasipokuwa wajanja, ashiki zinaweza kuwatumbukiza katika majuto.

“Wasichana wengi wanapata mimba wasizopanga kwa sababu ya hali hii. Wanahisi wamefika na kukosa kutumia kinga na watu wanaodhani wanawapenda kwa dhati kisha wanajipata kwenye mataa pindi tu wanapotangaza ni wajawazito. Majuto yanaanza na maisha yao yanabadilika wakiwa wazazi bila kutarajia,” asema Mithika.

Hii ndiyo hali ambayo Winfred* alijipata wakati mwanamume aliyekuwa akimkosesha usingizi akimuwaza alipoingia mitini baada ya kujua alikuwa amemtunga mimba.

“Mwanangu ana umri wa miaka minne sasa na sijawahi kumuona baba yake ambaye nilikuwa nimepagawa naye. Kama haingekuwa wazazi wangu, singemaliza masomo yangu chuoni,” asema Winfred.

Grace Alei, mwanzilishi wa Shirika la Salvage Love asema hatari za ashiki ni kubwa na nyingi kuliko raha inayozua.

“Unaweza kuvuruga maisha yako kwa sababu ya kupumbazika na kutawaliwa na hisia kuhusu mtu. Vijana wamevuruga masomo na hata kazi zao kwa sababu ya kulewa na ashiki wakidhani ni mapenzi ya dhati. Ukweli unapowabainikia, huwa wanajuta,” asema Alei.

Kuna njia ya kuepuka kuzama katika hali hii? Alei asema inahitaji mtu kudhibiti hisia zake na kufanya mambo kwa wakati na kipimo.

“Ukijali maisha yako kwanza, ukidhibiti hisia za mwili wako na ukijipenda kwanza, hautakosa usingizi au kuvuruga maisha yako kwa sababu ya mtu mwingine unayehisi kwamba hauwezi kuishi bila yeye. Ashiki ni tofauti na mapenzi ya dhati. Ni sawa na pombe ambayo ikiisha mwilini, mtu anajitambua na kujutia vitendo vyake akiwa mlevi,” ashauri Alei.

  • Tags

You can share this post!

WALIOBOBEA: Poghisio alivyoleta mageuzi katika sekta ya ICT...

BAHARI YA MAPENZI: Bosi wa kijakazi mume au mke?

T L