• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
PENZI LA KIJANJA: Usiwekeze hisia bila uhakika wa nia ya mpenzio

PENZI LA KIJANJA: Usiwekeze hisia bila uhakika wa nia ya mpenzio

NA BENSON MATHEKA

“SONGA mbele na maisha yako. Warembo hawajazaliwa bado, huyo hakuwa wako.”

Huu ulikuwa ushauri wa George kwa rafiki yake Jose baada ya kuachwa kwenye mataa na mpenzi wake wa miaka mitatu.

Jose alikuwa amesononeka kwa sababu ya hisia, muda, nguvu na pesa alizokuwa amewekeza kwa demu huyo kabla ya kumuacha ghafla.

“Kabla ya kumpata malkia wako, utabusu vyura wengi mwanamume wewe,” George alishauri Jose.

Makosa aliyofanya Jose, ni kudhani mwanadada huyo alikuwa na hisia sawa na zake kumhusu.

“Unaweza kuwa na hisia kali za mapenzi kwa mtu na mnaweza hata kulishana uroda lakini kusiwe na mapenzi ya dhati kati yenu. Hii ndiyo hali ambayo watu wengi hujipata wametumbukia na kuteseka,”asema mtaalamu wa mahusiano ya mapenzi Luka Sila.

Hisia hizi, asema, wakati mwingine huwa ziko na nguvu, sio kwa sababu ya mapenzi ya dhati mbali zinatokana na tamaa ya mwili.

“Katika hali hii, mtu anaweza kupata hasara akidhani eti kwa sababu anaburudishana na mwingine, kuna mapenzi ya dhati kati yao. Mapenzi ya dhati ni zaidi ya nderemo za chumbani,” asema Sila.

Mtaalamu huyu anaonya watu dhidi ya kuwekeza sana kwa washirika wao wa uroda kabla ya kung’amua iwapo kuna mapenzi ya dhati kati yao.

“Kuna kuwekeza kwa mshirika wako wa uroda na hakuumi kama kuwekeza kwa mtu ukidhani mtaoana. Muhimu ni kufahamu kutofautisha hisia za tamaa ya mwili na mapenzi ya dhati ili kuepuka masononeko,” asema Sila.

Kulingana na Mwanasaikolojia Franciscah Ulae, wa shirika la Maisha Mema jijini Nairobi, wanaume na wanawake wanaweza kupotoshwa na hisia za uroda na kufikiri wanaoburudishana nao wanawapenda kwa dhati na wangeoana.

“Mtu anayekupenda kwa dhati hana mbio ya kuchangamkia mwili wako. Hana tamaa ya uroda, kwanza anakujali na atataka kujua mengi kuhusu maisha na familia yako. Atazungumzia kuhusu mipango ya siku zijazo na hatakuwa na tamaa nyingi au kupenda anasa,” asema Ulae.

Mwanasaikolojia huyu anasema kinachofanya watu wengi kujuta ni kuamini kuwa anayekuonjesha tunda au kuchangamkia mwili wako ndiye anayekupenda kwa dhati.

“Uchu na tamaa ya mwili ni tofauti na penzi la dhati,” asema.

Wataalamu wanasema ili mtu aweze kuepuka masononeko akiachwa kwenye mataa na mpenzi wake, anafaa kuwa makini kabla ya kuwekeza hisia, muda na pesa.

“Unaweza kuwekeza kwa mtu ambaye mapenzi yake ya dhati yako kwa mtu mwingine kisha anapokuacha unaanza kulia hasara,” asema Ulae.

  • Tags

You can share this post!

KK, Azimio kupambana katika uchujaji wa mawaziri

Real Madrid wazamisha Getafe na kupaa hadi kileleni mwa...

T L