• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
KK, Azimio kupambana katika uchujaji wa mawaziri

KK, Azimio kupambana katika uchujaji wa mawaziri

NA ONYANGO K’ONYANGO

MIRENGO ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya sasa inajiandaa kukabiliana tena wiki ijayo kwenye kikao cha kuwapiga msasa mawaziri wateule.

Mirengo hii itapambana wiki hii baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kuamua kwamba Kenya Kwanza ndio mrengo wa walio wengi.

Wabunge wa Azimio wameahidi kuwakataa mawaziri wateule wanaokabiliwa na kesi mahakamani, wakisema Rais Ruto alidharau hitaji la katiba kuhusu maadili kwa kupendekeza majina yao.

Jana Jumamosi, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliambia Taifa Jumapili kwamba kwa sababu Kenya Kwanza imesema iko tayari kwa upinzani wenye nguvu, watafuatilia kwa makini ufaafu na maadili ya watu hao 23 waliopendekezwa kuketi katika baraza la mawaziri.

“Kwa hivyo, tutachunguza kwa makini maadili na uwezo wa watu hao waliopendekezwa na serikali hii. Naamini kuwa ikiwa wenzetu katika Bunge la Kitaifa wataheshimu kiapo chao cha kulinda katiba na hivyo kutupilia mbali majina ya wale wanaokabiliwa na mashtaka ya uhalifu,” akasema Bw Sifuna ambaye pia ndiye Katibu Mkuu wa ODM.

Kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi alisema watawatendea haki wote waliopendekezwa akionya kuwa wale wenye kasoro za kimaadili watakabiliwa na wakati mgumu watakapohitajika kujibu maswali fulani.

“Wengi wa walioteuliwa wamepungukiwa kimaadili na Rais anafahamu kasoro hiyo lakini akaamua kuipuuza kwa kuwasilisha majina yao bungeni. Hii ina maana kuwa serikali hii haithamini maadili na uwajibikaji,” akasema Bw Wandayi, ambaye ni mbunge wa Ugunja.

Akaongeza: “Wale wenye maadili ya kutiliwa shaka wanajijua. Wanafahamu madhara ambayo wameiletea nchi hii ndani ya miaka 10 iliyopita na tunataraji kuwa wamejiandaa kwa maswali makali ambayo tutawauliza.”

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na Mbunge wa Saboti Caleb Amisi jana waliongeza kuwa Azimio itaangazia suala la shahada ya digrii wakisema usimamizi wa rasilimali ya nchi hauwezi kuachiwa watu wenye masomo duni.

Hata hivyo, wakati huu hakuna sheria inayosema kuwa sharti mawaziri wawe ni watu waliohitimu kwa shahada za digrii.

Bw Kioni, ambaye ni mbunge wa zamani wa Ndaragua, akisema watahakikisha kuwa wale wenye kesi mahakamani hawaruhusiwi kushikilia nyadhifa za uwaziri nchini.

Bw Amisi alitisha kuwasilisha hoja ya kuwaondoa afisini mawaziri ambao wataidhinishwa licha ya kukabiliwa na kesi ya uhalifu kortini.

“Ikiwa Kenya Kwanza itatumia ushawishi wa Ikulu kupitishwa, ilivyo kawaida, tutawang’oa mamlakani mwezi mmoja baada ya kuapishwa kwao,” akasema Bw Amisi.

  • Tags

You can share this post!

Raila abuni mbinu mpya kujiimarisha

PENZI LA KIJANJA: Usiwekeze hisia bila uhakika wa nia ya...

T L