• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 2:53 PM
Penzi la mauti: Mume katili alivyoangamiza mke kwa kumdunga kisu mara kadhaa   

Penzi la mauti: Mume katili alivyoangamiza mke kwa kumdunga kisu mara kadhaa   

NA SAMMY WAWERU
KATIKA chumba kidogo cha kukodisha cha Christine Auma Odhiambo kilichoko mtaa wa Baba Dogo, Ruaraka, Nairobi tunaipata familia ya mama huyu ikiwa imelemewa na majonzi, kufuatia kifo cha bintiye kifungua mimba.
Akiwa ni mama wa watoto watatu anayetegemea vibarua vya kijungu jiko, Bi Auma alipoteza mwanawe, Viona Achieng, 23, mnamo Oktoba 23, 2023 usiku, baada ya kile kinachosemekana ni kudungwa na mume wake kwa kisu.  
Nyanyake Viona Achieng, Bi Florence Ngesa. PICHA|SAMMY WAWERU
Kisa hicho kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Ruaraka na kulingana na ripoti ya fomu ya upasuaji maiti, Achieng alifariki kutokana na mdungo wa kisu mara kadhaa.  
Tarehe ya mauaji iliyonakiliwa kwenye stakabadhi hiyo kubainisha kiini cha maafa, hata hivyo, inakinzana na siku wanayohoji wanafamilia mwana wao aliangamizwa.
Kwa mujibu wa fomu ya upasuaji maiti, Viona Achieng alikumbana na maafa Oktoba 24, 2023 na mwili wake ukapelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya City, Jijini Nairobi.
Nyanyake Viona Achieng, Bi Florence Ngesa akielezea kuhusu maafa ya kikatili ya mjukuu wake eneo la Baba Dogo, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU
Na huku wingu jeusi la simanzi likitanda na kutawala familia ya Bi Christine Auma, mshukiwa mkuu wa tendo hilo la kikatili na wahuni wenzake wangali huru.
“Tunachotaka ni haki itendeke. Ni huzuni kupoteza msichana mwenye umri mdogo kama mjukuu wangu,” alisema nyanyake Achieng, Bi Florence Ngesa alipozungumza na Taifa Leo Dijitali kwa niaba ya familia. 
Nyanyake Viona Achieng, Bi Florence Ngesa akionyesha stakabadhi za ukaguzi wa kiini cha maafa ya mjukuu wake na cheti cha mochari. PICHA|SAMMY WAWERU
Msichana huyo ambaye ni mama wa watoto wawili, amekuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka minne na mumewe aliyetambuliwa kama Nicholas Ouma Ochieng almaarufu Ouna.
Achieng alikumbana na mauti eneo la Kariadudu, Baba Dogo mita chache kutoka anakoishi mamake.
Chumba kidogo ambapo Viona Achieng alihamia na wanawe wawili, kuishi na mamake, Christine Auma baada ya mzozo kati yake na mumewe uliosababisha maafa yake. PICHA|SAMMY WAWERU
Ndoa yake ikitajwa kusheheni migogoro, shangaziye Marion Atieno alifichua kuwa kabla kuuawa alikuwa ametengana na mshukiwa miezi miwili iliyopita.
“Kabla ya kuuawa, mumewe alichukua mmoja wa watoto wao kisha akamhadaa amuendee usiku. Alitumia mwanya huo kumwangamiza,” Bi Atieno alisimulia.
Shangaziye Viona Achieng, Marion Atieno akisimulia jinsi mpwa wake alikumbana na mauti mikononi mwa mumewe katili. PICHA|SAMMY WAWERU
Cha kushangaza zaidi, inasemekana mshukiwa ambaye kwa sasa angali mafichoni, alisaidiwa kutekeleza unyama huo na marafiki wenzake wawili ambao wangali huru.
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCIO) Kaunti Ndogo ya Starehe, David Cheruiyot kwenye mahojiano na Taifa Leo alisisitiza kwamba makachero wanaendelea kumsaka.
“Uchunguzi unaendelea na pindi tutakapokamata mshukiwa mkuu, tutamfungulia mashtaka – Faili ikiidhinishwa na Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODPP),” Bw Cheruiyot akasema.
Tayari mashahidi kadha wameandikisha taarifa, na kisheria ODPP anapaswa kukagua faili ya uchunguzi kabla kutoa mwelekeo.
Nyanyake Viona Achieng, Bi Florence Ngesa aonekana kulemewa na majonzi baada ya kupoteza mjukuu wake. PICHA|SAMMY WAWERU
Endapo atashawishika na ushahidi, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) ataagiza mshukiwa au washukiwa kufunguliwa kesi mahakamani na kukumbana na makali ya sheria.  
Huku oparesheni kutia nguvuni mshukiwa mkuu ikiendelezwa, DCIO Cheruiyot ameomba umma wenye taarifa itakayowezesha makachero kukamata mumewe Achieng, kuiwasilisha katika chochote cha polisi kilicho karibu.
Ripoti ya ukaguzi kubaini kiini cha maafa ya Viona Achieng, anayesemekana kuuawa mikononi mwa bwanake. PICHA|SAMMY WAWERU
Tetesi zikihoji mmoja wa waliosaidia Nicholas Ouma Ochieng kuangamiza mkewe alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Ruaraka, na hatimaye kuachiliwa huru baada ya mwanasiasa maarufu Baba Dogo kutumia ushawishi wake, Bw Cheruiyot alitupilia mbali madai hayo akiyataja kama ‘yasiyo na msingi wowote’ kwani kesi ya mauaji ni kati ya zenye uzito na zisizotaka mzaha.
Cheti cha mochari ya City, Nairobi ambapo mwili wa Viona Achieng ulipelekwa baada ya kuuawa kinyama eneo la Baba Dogo mikononi mwa mumewe katili. PICHA|SAMMY WAWERU
Bi Christine Auma Odhiambo akisubiri kupata haki, kupitia mahojiano kwa njia ya simu alisema anahangaika kupata fedha kusafirisha mwili wa bintiye Siaya kwa minajili ya mazishi.
Baba Dogo na mitaa jirani kama vile Lucky Summer na Mathare, visa vya mauaji na uhalifu vinazidi kukithiri.
 
 
 
  • Tags

You can share this post!

Naisula Lesuuda kati ya wabunge 10 bora wa kike wanaochapa...

Wizi: Madereva wa matrela wanavyolazimika kulala mvunguni...

T L