• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
RIWAYA: Sifa za Neema na jinsi anavyoendeleza ploti katika Chozi la Heri

RIWAYA: Sifa za Neema na jinsi anavyoendeleza ploti katika Chozi la Heri

JUMA lililopita tulijadili sifa za Mwangemi na umuhimu wake.

Leo tutamhakiki Neema, mkewe Mwangemi na mamake wa kupanga wa Mwaliko.

Neema alijaliwa kumpata mwana mmoja, Bahati na aliyeaga dunia kabla ya kutimiza hata juma moja ulimwenguni kutokana na ugonjwa wa “sickle cell”

SIFA ZAKE

Mwenye upendo, anamlea Mwaliko kwa upendo licha ya kukosa kuwa na mwanawe wa kumzaa. Hali hii inamchochea Mwaliko kuhisi kuwa analo deni kubwa la kumlipa kwa sababu ya upendo mkuu kwake.

Mwenye utu, anamchukua na kumlea Cynthia wazazi wake wanapoaga dunia. Pia alimuokoa mtoto Riziki Immaculata, aliyekuwa ametupwa kwenye biwi la taka licha ya kuonywa na mpitanjia dhidi ya kubeba mzigo usio wake.

Mwenye majuto, tunamuona akisikitika baadaye anaposhauriwa na Mwangemi kumpanga mwana, anakumbuka majadiliano aliyokuwa nayo na Mtawa Cizarina “Hadi sasa najutia kutouzingatia ushauri wa Cizarina… “uk163.

Mwenye utani/ucheshi, Mwaliko alipomkataza kuandamana nao mjini kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Mwangemi, anamtania kwa kumwambia kuwa labda alitaka kumleta mkaza mwana lakini aliogopa kwamba huenda mama mtu akamchambua asimbakize.

Mwenye heshima, aliheshimu uamuzi wa Mwaliko wa kutoandamana nao mjini.

Mlezi mwema, alishirikiana na mumewe kumlea Mwaliko ipasavyo hadi akawa mwenye nidhamu, akiwaheshimu wazazi wake, majirani na kuwatii walimu wake.

Mwajibikaji, alikiokota kitoto kilichotupwa jaani na kukipeleka kwenye kituo cha polisi.

UMUHIMU WAKE

Ametumika kuendeleza ploti ya riwaya hii kwa kuzua matukio kadhaa mathalan suala la ukiukaji wa haki za watoto linajitokeza anapokiokota kitoto kilichorushwa jaani.

Pia sauti ya mpitanjia inadhihirisha kwamba uozo huu umekithiri anapomwambia Neema asishughulike na kujipagaza mzigo usio wake kwani ni vijusi vingapi vilitupwa pale vikajifia. Inadhihirika kuwa mpitanjia ni katili.

Anaendeleza maudhui ya uwajibikaji. Alikiokoa kitoto kilichotupwa kwenye jaa na kukiondolea maafa yaliyokichungulia.

Kielelezo cha utu. Alimlea mpwawe Cynthia baada ya wazazi wake kuaga dunia. Pia anamwokota mtoto kwenye biwi la taka.

Anaonyesha umuhimu wa mashirika yanayoshughulikia huduma za kimsingi kwa watoto waliohiniwa haki zao mathalan makao ya Benefactor yanatoa hifadhi na elimu kwa watoto waliotelekezwa katika jamii kama vile Riziki na Mwaliko. Aidha, yanasaidia jamii zisizojaliwa kupata watoto kupanga mwana kama alivyofanya Mwangemi na Neema.

Anabainisha dhiki za wanawake walio na matatizo ya kuzaa. Wanajamii walimcheka na kumkejeli kwamba alishindwa kulea hata mimba na wengine wakasema kuwa alizaa watoto wenye upungufu kwa sababu aliavya mimba nyingi akiwa shuleni.

Tathmini-Jadili namna ambavyo Mwaliko anaendeleza maudhui ya ukiukaji wa haki za watoto.

Joyce Nekesa

Kapsabet High School

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Uandishi ndio njia aula zaidi ya kuacha...

VYAMA: Chama cha Uanahabari katika Shule ya Upili ya St...

T L