• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
KAULI YA MATUNDURA: Uandishi ndio njia aula zaidi ya kuacha taathira maishani

KAULI YA MATUNDURA: Uandishi ndio njia aula zaidi ya kuacha taathira maishani

NA BITUGI MATUNDURA

MNAMO 2017, niliwasiliana na mchapishaji wangu – Phoenix Publishers, Nairobi na kuonesha azma ya kufanya marekebisho kwenye novela yangu, Mkasa wa Shujaa Liyongo.

Novela hii, niliyoitunga nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Moi mnamo 1998, ni mojawapo ya tungo zangu za kifasihi zenye ‘umaarufu’.

Dhana ya ‘umaarufu’ katika mktadha huu inaumana na upokezi na mwitiko wa wasomaji, na idadi ya mauzo.

Kazi hii iliyochapishwa 2001 kwenye msururu wa ‘Hadithi za Kikwetu’, na kuidhinishwa na Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala ya Kenya (KICD), imekwisha kuchapwa upya (reprinted) mara kumi.

Novela hii ni usimilisho wa Utenzi wa Fumo Liyongo (M.Kijumwa).

Sababu ya kuifanyia marekebisho novela yangu ilitokana na msukumo kwamba, mhariri hakuitendea haki.

Ilisadifu mchapishaji alikuwa ametambua udhaifu huo, na akaridhia ombi langu. Toleo la mwaka 2018 sasa ni kazi safi.

Ingawa mchakato tulioufanya kukiboresha kitabu hicho ni muhimu, kilichoteka nyara akili zangu ni majina ya baadhi ya waandishi waliochangia msururu wa Hadithi za Kikwetu waliokwisha kufariki. Hawa ni pamoja na P.M. Kareithi (Kaburi Bila Msalaba ), Jay Kitsao (Kishu Kazi), Njiru Kimunyi (Mlima Kenya Kajifungua), Leo Odera Omolo (Tajiri Mjanja), Ken Walibora (Mtu wa Mvua), Catherine Kisovi (Mama wa Kambo) na Fortunatus Kawegere (Kinga ya Rushwa).

Ingawa waandishi hawa wamekwisha kufariki, mchango wao katika fasihi ya Kiswahili – na hasa utanzu wa fasihi ya watoto ,utaendelea kuacha taathira kubwa.

Chambacho wahenga, liandikwalo halifutiki.

  • Tags

You can share this post!

USHAURI NASAHA: Yazue mabadiliko chanya masomoni mwako...

RIWAYA: Sifa za Neema na jinsi anavyoendeleza ploti katika...

T L