• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
RIWAYA: Umuhimu wa Ridhaa kukuza maudhui na kuendeleza ploti

RIWAYA: Umuhimu wa Ridhaa kukuza maudhui na kuendeleza ploti

BAADA ya kushughulikia sifa za Ridhaa Alhamisi iliyopita, leo hii tutajadili kwa kina nafasi anayowakilisha katika kujenga ploti na kuendeleza maudhui mbalimbali yanayojitokeza riwayani.

Ridhaa ametumika kuendeleza maudhui ya madhara ya ukabila.

Hali hii inajitokeza wakati jumba lake pamoja na aila yake isipokuwa Mwangeka inateketezwa na jirani yao Mzee Kedi baada ya vurugu za baada ya uchaguzi kwa tuhuma kwamba walikuwa wageni hapo na kuwa walionekana kuwanyang’anya wenyeji mashamba yao.

Anaendeleza maudhui ya malezi mema jinsi anavyoshirikiana na aila yake. Mathalan, kupitia mbinu rejeshi tunaona jinsi alivyomlea Tila.

Wana mazungumzo pevu na vilevile anamshauri Mwangeka kuhusu sehemu ambayo anastahiki kununua shamba.

Aidha, Ridhaa anaishi na Mwangeka ili kumsaidia kukabiliana na jakamoyo la kupoteza familia yake. Ridhaa anapomwona Mwangeka ametulia katika ndoa na Apondi, anawaachia nafasi ya kuishi vizuri.

Anaendeleza maudhui ya ushirikino pale ambapo anahusisha matukio kama milio ya kereng’ende na bundi usiku na mbiu ya mgambo ambayo ingezua jambo.

Uhafidhina

Vilevile, anaashiria uhafidhina pale ambapo mamake anamjuza kuwa mwanamume hafai kulia hata mbele ya majabali ya Maisha.

Kupitia kwake, tunajuzwa kuhusu jinsi ukoloni na ukoloni mbamboleo uliwakandamiza wahafidhina. Kuwa walinyang’anywa mashamba na wakoloni wakaanzisha hati miliki na wale ambao walikosa pesa walipokonywa mashamba.

Ridhaa ni mtu wa kuwapa wengine matumaini, ndiposa anajenga hospitali ya Mwanzo Mpya ili kuwahudumia wahafidhina wote bila kujali asili wala fasili yao.

Ridhaa anasawiri jinsi uongozi mbaya unaovyoendeleza uharibifu wa mali. Majumba yake na ya wenzake yanaharibiwa kwa sababu ya kujengwa katika sehemu iliyotengewa njia. Serikali ilikuwa wapi majumba haya yakijengwa?

Ridhaa pia anaendeleza ploti kwa kutujuza matukio mbalimbali ambayo yametukia katika riwaya hii kama vile familia yake kuhamishwa hadi msitu wa Heri, namna babake alivyokuwa na wake kumi na wawili, masomo yake, alivyonawiri kikazi, kuweza kuhamasisha wananchi kuhifadhi mazingira, kutujuza kuhusu mahusiano na majirani wake.

Migogoro

Kimsingi, anaonyesha migogoro inayozuka riwayani na hata mbinuishi zinazochukuliwa na Wahafidhina kuimarisha Maisha yao baada ya changamoto walizozipitia.

Ametumika pia kujenga wahusika wengi sana. Kupitia kwake, tunajua sifa za babake Mwimo Msubili aliyekuwa na wake kumi na wawili, tunajuzwa uhafidhina wa mamake, tunajuzwa asante ya punda ya Mzee Kedi, tunajuzwa kuhusu Tila – msichana aliyepevuka kimawazo licha ya kuwa na umri mdogo, kujuzwa kuhusu usuhuba na mahaba yake kwa Terry.

Almradi, Ridhaa ametuwezesha kuwatambua wahusika wengi aliohusiana nao kwa njia moja au nyingine.Swali la tathmini: Eleza jinsi Ridhaa ametumika kuboresha maisha ya wahafidhina?

 

Swali la tathmini: Eleza jinsi Ridhaa ametumika kuboresha maisha ya wahafidhina?

Joyce Nekesa

Kabsabet Boys High School

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Sheng inafaa kupigwa marufuku miongoni mwa...

Liverpool yapiga Southampton na kulazimisha mshindi wa EPL...

T L