• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Ruto aonywa kuhusu mpango wa kuwaondolea wageni viza

Ruto aonywa kuhusu mpango wa kuwaondolea wageni viza

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI imetahadharishwa dhidi ya kutekeleza mpango wake wa kuondoa hitaji la viza dhidi ya raia wote wa kigeni watakaoingia nchini, kuanzia Januari 2024.

Tangazo hilo lilitolewa na Rais William Ruto, Jumanne, Desemba 12 alipowaongoza Wakenya kuadhimisha Sikukuu ya Jamhuri 2023.

Kwenye hotuba yake, Rais Ruto alisema kuwa mpango huo unalenga kuipa nafasi Kenya kupata maendeleo na ustawi wa kiuchumi kutoka kwa mataifa yale mengine.

“Mataifa mengi duniani yamejinyima nafasi za maendeleo kupitia vizingiti vinavyotokana na hitaji la watu wanaoingia humo kuwa na viza. Sisi tunataka kujitoa kwenye mtego huo,” akasema Rais Ruto.

Licha ya mpango huo, wadadisi wa mahusiano ya kimataifa wanasema Kenya inahitaji kuchukua tahadhari kubwa kabla ya kuanza kutekeleza mpango huo.

Kulingana na Profesa Peter Kagwanja, ambaye ni mdadisi wa siasa na msomi wa mahusiano ya kimataifa, ingawa hatua hiyo ni nzuri kwa ustawi wa kiuchumi wa Kenya, serikali haifai kuharakisha utekelezaji wake.

“Bila shaka, huu ni mpango mzuri, kwani lengo lake kuu ni kuifungua Kenya kwa mataifa mengine ili kuwapa raia wake nafasi ya kutalii na kuwekeza nchini. Ni mpango unaolenga kuifananisha Kenya na mataifa ya Umoja wa Ulaya (EU), kwani huwa yanatumia viza moja. Hata hivyo, lazima tutahadhari, hasa kutokana na changamoto za kiusalama ambazo zimekuwa zikitukumba hapo awali,” akasema Profesa Kagwanja.

Kulingana na msomi huyo, lazima Kenya izingatie baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiiandama, kwa mfano; tishio la ugaidi kutoka kwa makundi ya wanamgambo kama vile Al-Shabaab.

“Kwa mpango huo kufaulu, lazima serikali iimarishe mikakati ya kukabiliana na ukosefu wa usalama na kuhakikisha kuwa hatua hiyo haitaifanya Kenya kuwa kitovu cha uendeshaji wa maovu kama ulanguzi wa pesa na binadamu,” akasema Prof Kagwanja.

 

  • Tags

You can share this post!

Mwanariadha Kiptum alivyochangamsha watu Monaco akihutubu...

Demu akubali mistari ya jamaa kwa sharti moja: “Utanilipa...

T L