• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Seneta Methu: Wanaopinga Mswada wa Fedha 2023 ni sawa na wahanga wa Shakahola wasioelewa Biblia   

Seneta Methu: Wanaopinga Mswada wa Fedha 2023 ni sawa na wahanga wa Shakahola wasioelewa Biblia  

NA SAMMY WAWERU

HUKU Wakenya wakiendelea kubanwa na gharama ya juu ya maisha hasa baada ya Mswada wa Kifedha 2023 kuidhinishwa na Rais William Ruto kuwa sheria, seneta wa Nyandarua John Methu amedai baadhi ya mapendekezo ya mswada huo yalitolewa kwenye Biblia.

Akielezea kushangazwa kwake na wanaopinga mswada huo, mwanasiasa huyo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alisema haelewi dini ambalo wanaoupinga wanaabudu.

“Ningetaka kujua wanaopinga Mswada wa Fedha 2023 ni wa dini gani, kwa sababu baadhi ya mapendekezo yalitolewa kwenye Biblia,” alihoji seneta huyo mnamo Jumapili, Julai 2, 2023.

Akiwalinganisha na wahanga wa mkasa wa Shakahola, Bw Methu aliwahimiza kuchambua Biblia akihoji vigezo vilivyomo kwenye Kitabu hicho Takatifu vilijumuishwa kwenye mswada wa fedha.

“Wanaoupinga ni sawa na waathiriwa wa Shakahola, ambao hawaelewi Biblia. Yesu alisema yeye ndiye atatujia, ilhali wao walikuwa wanajinyima chakula na maji ili wakutane na Yesu.”

Alitoa matamshi hayo katika ibada ya misa Kanisa la St Mary’s Molo, Nakuru ambayo pia ilihudhuriwa na Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Seneta huyo hata hivyo hakutoa mfano wa Biblia aliodai mchango wake ulitumika kwenye Mswada wa Kifedha 2023.

Mswada huo ambao Dkt Ruto aliutia saini kuwa sheria unapendekeza nyongeza ya ushuru, hatua ambayo wanauchumi wameonya itachangia maisha kuwa magumu.

Muungano wa Azimio, unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga umetishia kuandaa maandamano Ijumaa, Julai 7, 2023 Sikukuu ya Sabasaba Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Samidoh analenga kiti cha kisiasa 2027?

Msako wa walioua kinyama Kaniss na Omodollar na kuweka...

T L