• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
SHANGAZI SIZARINA: Nina wasiwasi kumhusu binti yangu, amepoteza uchamgamfu wake, kunani?

SHANGAZI SIZARINA: Nina wasiwasi kumhusu binti yangu, amepoteza uchamgamfu wake, kunani?

MIMI ni mama wa msichana wa umri wa miaka 11 ambaye anasoma shule ya msingi ya bweni.

Wakati msichana wangu alirudi likizo niligundua mabadiliko ya tabia yake kiasi kwamba inanitia mashaka. Awali binti yangu alikuwa mchangamfu sana na alikuwa anapenda kuzungumza kila wakati.

Hata hivyo wakati huu alikuwa kimya sana na akawa anajifungia chumbani muda mwingi. Na hata nilipojaribu kuzungumza naye, hakuwa mchangamfu kama nilivyomzoea.

Nimejaribu kuongea naye na kumuuliza iwapo ana shida yoyote, lakini ameniambia hana shida.

Nina mashaka kwani mwanangu hakuwa hivi awali. Tafadhali nishauri nifanyeje, kwani sina amani kabisa.

Dada, ni vyema kwamba umekuwa na wakati wa kutathmini mwenendo na tabia ya mwanao na hata kuzungumza naye. Mtoto anapobadilika tabia ghafla, mara nyingi huwa ni dalili za awali ya mambo aliyotendewa ama pia yale ambayo anapitia. Nadhani itakuwa vyema umtembelee huko shuleni anakosoma na uzungumze na walimu wake, uelewe mazingira anayolala, watu anaolala nao na hata wale walio karibu naye kila siku. Kifupi ni kwamba chukua hatua sahihi mapema ili kuweza kumnusuru mwanao na yale ambayo anapitia ambayo huenda yakaathiri maisha yake ya sasa na hata baadae.

Nimekataa kumpa burudani kabla ndoa sasa anadai simpendi

Mimi ni mwanamke wa umri wa miaka 25. Pia nina mtoto mmoja. Nilimkimbia mume wangu kwa kutokuwa mwaminifu. Sasa nimepata mchumba ameniahidi kunioa. Lakini anasisitiza ngono kwanza. Nimekataa, anasema simpendi. Nifanyeje?

Ni vizuri kuonyesha msimamo wako tangu mwanzo wa uhusiano. Na kama kweli huyo mwenzako anakupenda kwa dhati, atapenda kujua sababu ya kukataa kufanya mapenzi kabla ya ndoa na labda mnaweza kufikia makubaliano ya pamoja kuhusiana na suala hilo.

Nifanyeje na nampenda?

Mimi ni kijana wa umri wa miaka 23. Kuna msichana nampenda sana. Baada ya kukaa naye kwa muda, nasikia ana mpenzi mwingine. Nilimuuliza, akakana. Siku moja nikiwa naye, akatokea jamaa mmoja na msichana akakimbia na kuniacha peke yangu. Nifanyeje na nampenda sana?

Ni mawili, huyo jamaa ni mpenzi wake ama ni ndugu yake. Chunguza na umwulize kwa nini alikimbia alipomuona huyo mwanaume.

Roho imependa wa pembeni, mke atakubali mwenza?

Mimi ni kijana ambaye nimeoa. Lakini nampenda msichana mwingine na nafikiria kumwoa. Lakini namwogopa mke wangu. Je, nikimweleza mke wangu nataka kuoa mke mwingine atakubali? Naomba ushauri.

Mimi siwezi kujua kama atakubali ama atakataa. Hiyo ndoa yenu mlifungaje? Ilikuwa ya mke mmoja ama inaruhusu wake wengi? Jambo la muhimu zungumza naye ndipo utajua msimamo wake. Lakini pia uwe tayari kwa lolote litakalotokea.

Watoto wa mpenzi wanidharau, nifanyeje?

Nina mpenzi ambaye nampenda sana na ana watoto wawili ambao alizaa na mume na akafa. Sasa nikiwaambia chochote wanasema mimi sio baba yao. Nishauri.

Kwa hiyo uhusiano wako na mama wa hao watoto ni wa kimapenzi tu na wala sio ndoa? Hiyo lazima ilete changamoto, kwani watoto hao huenda wanahisi kuporwa mapenzi ya mama yao. Muhimu ni kwamba usilazimishe uhusiano, bali nenda taratibu ili uweze kuunda imani yao kwako.

  • Tags

You can share this post!

HUKU USWAHILINI: Leo nakupasha ya Andunje, mfupi wa kimo...

MALEZI KIDIJITALI: Kumkinga na hatari ibuka za mtandao

T L