• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
SHINA LA UHAI: Tahadhari minyoo huathiri wakubwa kwa wadogo

SHINA LA UHAI: Tahadhari minyoo huathiri wakubwa kwa wadogo

NA WANGU KANURI

WAKENYA zaidi ya milioni 10 wanaugua maradhi ya minyoo huku wengine milioni 16 wakiwa kwenye hatari ya kuugua maradhi haya, takwimu kutoka Wizara ya Afya nchini, zimeonyesha.

Licha ya maradhi haya kuathiri wakubwa kwa wadogo, wake kwa waume, kina mama wajawazito wanaweza kupunguza hatari ya mtoto kufariki kwa asilimia 14 katika wiki nne za kwanza baada ya kuzaliwa.

Hata hivyo, ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa ambayo yamepuuzwa duniani (Neglected Tropical Disease) na kwa hivyo maradhi haya hayajapewa kipaumbele na serikali.

Minyoo ni maradhi yanayoenezwa na vimelea haswa katika maeneo yenye joto jingi kwa mfano kaunti za Mombasa, Lamu, Wajir, Mandera na Malindi pamoja na maeneo mengine yenye hali hii ya anga.

Minyoo huenezwa baada ya mayai yaliyopo kwenye kinyesi cha binadamu au wanyama wengine walio na maradhi hayo kuanguliwa kwenye udongo au mazingira duni.

Hata hivyo, maambukizi hayo huchukua kipindi cha wiki tatu kabla ya kuathiri watu na dalili za kuugua kwake kuanza kujitokeza.

Hii ni kwa sababu mayai yanayoanguliwa huhitaji kipindi cha angalau wiki tatu kukua ili kuweza kuambukizana.

Kuna aina nne za vimelea; wale wanaopatikana katika utumbo (intestines) wa wanyama (roundworms), wale wanaopatikana katika utumbo mkubwa (whipworm) na wale wanaoingia kwenye ngozi (roundworms) baada ya kutembea miguu tupu kwenye mazingira yaliyo na vimelea hivi.

Kwa mujibu wa Dkt Florence Wakesho, mtaalamu wa masuala ya vimelea katika Wizara ya Afya, maambukizi haya huenea sana haswa kwenye maeneo yasiyo na maji ya kutosha au sehemu ambapo hakuna mazingira safi.

“Mtu anaweza akaugua minyoo baada ya kula vyakula vilivyoathiriwa na vimelea hivyo,” anasema.

Watoto huwa kwenye hatari zaidi sababu ya kucheza na maji au kula vyakula viliyoathiriwa na mayai yaliyoanguliwa na vimelea, na kula kabla ya kuosha mikono.

Minyoo hiyo hunyonya damu za mnyama au mwanadamu waliovamia na kusababisha upungufu wake mwilini.

Dalili za mgonjwa wa minyoo ni kuendesha, kuhisi uchovu, kuwa na maumivu, kupoteza uzito na kuwa na upungufu wa damu mwilini.

“Minyoo haswa ile inayopatikana kwenye utumbo (intestines) inapokuwa kwa wingi mwilini, mgonjwa huyo hutibiwa kwa kufanyiwa upasuaji,” anasema Dkt Wakesho.

Maradhi haya yanaweza yakazuiwa iwapo watu watazingatia uoshaji wa matunda na mboga kwa maji safi kabla kula, kunawa mikono kwa maji na sabuni baada ya kujisaidia na kabla ya kula chakula na matumizi mazuri ya vyoo.

Mwaka 2022, Wizara ya Afya iliripoti kuwa, angalau Wakenya milioni 20 walikuwa na minyoo.

Kwa mujibu wa Dkt Wycliff Omondi, Mkuu wa Idara ya Kushughulikia Maradhi Yaliyopuuzwa katika Wizara ya Afya, kaunti 27 zilirekodi idadi kubwa ya wagonjwa wa minyoo.

“Tunaangazia jinsi tutaweza kukabiliana na minyoo haswa katika sehemu mbalimbali za nchi zilizo na visa vingi vya wagonjwa wa minyoo haswa, maeneo ya kati, mashariki, magharibi mashariki na magharibi mwa nchi. Tunaangazia kumaliza magonjwa ya NTD ifikapo 2025.”

Isitoshe, serikali kupitia mradi wa Kuangamiza Minyoo Shuleni (NSBDP), ilianzisha mpango maalum unaolenga kuwapa watoto milioni sita kote nchini dawa za kuangamiza minyoo.

Mradi huo ulinuiwa kunufaisha watoto wenye umri wa kati ya miaka 2-14 katika kaunti zote nchini.

Aliyekuwa waziri msaidizi wa afya, Dkt Rashid Aman, aliwahi kunukuliwa, akisema kuwa watoto zaidi ya milioni sita wanakabiliwa na tishio la maambukizi kila mwaka.

Utafiti uliofanywa na wizara hiyo kati ya miaka ya 2019 na 2022, ulionyesha kuwa kaunti ya Lamu ndiyo inaongoza kwa idadi kubwa ya visa vya minyoo kwa asilimia 13.

Kaunti ya Vihiga inafuatia kwa asilimia 11, Kwale (9%), Kakamega na Tana River (8%), Kilifi na Bungoma (7%), Siaya (6.1%), Migori (5.2%), Busia (5.1%), Trans Nzoia (5%), Mombasa (4%), Homa Bay (2.9%), Kisumu (2.1%) na Taita Taveta (1%).

Mnamo 2021, Wizara ya Afya iliwapa Wakenya wanaoishi katika kaunti za Vihiga, Bungoma, Kakamega na Trans Nzoia dawa za minyoo.

Kulingana na utafiti uliofanywa na wizara hiyo katika wadi 155 za kaunti hizo nne, watu kutoka wadi 140 walikuwa na minyoo.

“Katika kaunti ya Bungoma pekee, tuliwatibu watu 1.5 milioni ambao wapo kwenye hatari na wengine 600,000 kutoka kaunti ya Vihiga,” akasema Bi Wakesho.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watoto karibu milioni 900 wanakabiliwa na tishio la kuambukizwa minyoo.

Isitoshe, watu 1.5 bilioni , takribani asilimia 24 ya watu wote duniani, huathiriwa na minyoo.

Maradhi yanayotokana na minyoo yameripotiwa kusababisha vifo 405,000 huku wengine 37 milioni wakipata ulemavu kila mwaka.

Licha ya kuwa kumeza dawa za minyoo ni suluhisho katika kupambana na minyoo, suluhu ya kudumu inaweza kuafikiwa iwapo watu watazingatia usafi, wataalam wanaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Mazungumzo: Raila na Ruto walaumiana

Tunatathmini mashtaka ya kumfungulia Mackenzie – Haji

T L