• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
SHINA LA UHAI: Tatizo la kigugumizi linakumba zaidi watoto wa kiume

SHINA LA UHAI: Tatizo la kigugumizi linakumba zaidi watoto wa kiume

NA PAULINE ONGAJI

NI miaka 15 sasa tangu Dennis Kibandi Mbugua, mkazi wa Thika, Kaunti ya Kiambu, agundulike kuwa na tatizo la kigugumizi, na hali hii sio rahisi kwa kijana huyu anayejaribu kuimarisha kipaji chake kama mwanamuziki.

“Sio rahisi unapojaribu kuzungumza ambapo kila mara unaharakisha kuzungumza ili angalau uweze kuvuta hewa,” aeleza.

Ni tatizo ambalo Bw Mbugua anasema limemletea masaibu tele tokea utotoni kwani liliathiri mawasiliano na watoto wenzake, na hata masomo yake alipojiunga na shule ya msingi.

“Nakumbuka kuna wakati ambapo ningeinua mkono darasani nikitaka kujibu swali, ila tu kunyimwa fursa hiyo na mwalimu kwa sababu ya udhaifu uliokuwa ukinikumba,” asimulia.

Mambo yalikuwa mabaya hata zaidi alipojiunga na shule ya upili ambapo kuna baadhi ya wanafunzi ambao wangemdhihaki.

“Changamoto ilizidi alipohitajika kusoma kwa sauti darasani. Ni walimu wachache waliokuwa na uvumilivu wa kuniruhusu nisome polepole,” aeleza.

Mpaka sasa anaendelea kukabiliana na changamoto hii hasa anapowasiliana na watu ambao hawafahamu hali yake.

“Ni changamoto kubwa hasa ninapozungumza na watu wasiofahamu hali yangu, na mara nyingi najipata nikishindwa kuwajibu wanaponiuliza maswali, ” aeleza.

Aidha, hali hii imekuwa kizingiti katika taaluma yake kama mwanamuziki.

“Kutokana na sababu kuwa mimi ni muimbaji, kuna wakati ambapo nikiwa kwenye studio nashindwa kutamka baadhi ya maneno na mara nyingi hujawa na hofu na kunyamaza.Kuna wakati ambapo hali hii humuudhi na kumkasirisha produsa,” aeleza.

Shida hii ilimuanza ghafla akiwa mtoto mdogo na kuthibitishwa akiwa na miaka mitano pekee. Hii iliwashtua wazazi wake na kuwashinikiza kuanza kumtafutia matibabu mara moja.

Alipelekwa katika hospitali tofauti, lakini tatizo ni kwamba kote alikoenda, madaktari walikuwa na maelezo tofauti kuhusu hali yake.

“Kuna wale waliosema kwamba kimeo changu ni kirefu au kizito, huku wengine wakiashiria kwamba ulimi wangu ulikuwa mzito. Hata kunao waliohoji kwamba mafindo yangu yalikuwa na matatizo,” aeleza

Hata hivyo, baada ya kuchoshwa na maoni tofauti kila walipoenda hospitali, familia yake iliamua kusalimu amri na kuanza kutafuta mbinu za kuidhibiti hali hii.

Kulingana na wataalamu, kigugumizi ni hali ya kinyurolojia ambapo mabadiliko madogo kwenye ubongo husababisha matatizo ya kuzungumza.

Katika hali hii, mwathiriwa hurudia sauti, silabi au maneno, kurefusha sauti na kukatiza mfululizo wa kunena.

“Mwathiriwa kwa kawaida hujua kitu anachotaka kusema lakini hushindwa kutoa matamshi kwa mfululizo,” aeleza Dkt Catherine Nzau, mtaalamu wa tiba ya matatizo ya kunena.

Kulingana na Dkt Nzau, kwa sababu ya kukatizwa wakati wa kunena, mara nyingi ataonekana aking’ang’ana kwa kupepesa macho au kutetemesha mdomo.

“Hali hii yaweza fanya iwe ngumu kwake kuwasiliana na watu wengine, na hivyo kuathiri ubora wa maisha yake,” aongeza Dkt Nzau.

Hapa nchini, hakuna takwimu thabiti zinazoonyesha ni watu wangapi wanaokumbwa na hali hii. Hata hivyo, kimataifa, data za wanasayansi zinaonyesha kwamba kigugumizi hukumba watu wa umri wote, lakini hasa hutokea miongoni mwa watoto kati ya umri wa miaka miwili na sita, kutokana na sababu kuwa wanakuza ujuzi wa kuzungumza.

Kulingana na wataalamu, takriban asilimia 8 ya watoto (wavulana na wasichana) kati ya miaka miwili na mitano watakumbwa na kipindi kifupi maishani cha kugugumiza.

Kipindi hiki, wanasema, huwa miezi kadhaa, ambapo kugugumiza kutatokea na kutoweka. Lakini endapo hali hii itaendelea kufikia umri wa kukomaa, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba itadumu.

Takwimu zinaashiria kwamba wavulana hukumbwa na kigugumizi kati ya mara mbili na tatu zaidi ya wasichana, na wanapoendelea kukua, pengo la kijinsia hupanuka.

Aidha, idadi ya wavulana wanaoendelea kuathirika maishani ni mara tatu au nne zaidi ya wasichana.

Takriban asilimia 75 ya watoto walioathirika hupona hali hii miaka inavyozidi kusonga.

Kulingana na watafiti wa kimatibabu, hali hii hurithiwa ambapo asilimia 60 ya wathiriwa wana jamaa kwenye familia anayekumbwa na shida hii.

Lakini kuna aina nyingine ya kigugumizi ambayo ni nadra na hutokea katika miaka ya ukomavu ambayo kwa jina la kitaalamu inafahamika kama acquired stammering au adult onset stammering.

Sababu kuu hapa huwa jeraha la kichwa, kiharusi au maradhi ya mfumo wa neva kama vile Parkinson’s Disease.

Sababu zingine zaweza kuwa msongo wa akili au matumizi ya aina fulani ya dawa.

Kwa sasa hakuna dawa kamili za kutibu kigugumizi bali kuna aina mbali mbali za matibabu zinazotumika kudhibiti ishara zinazotokana na hali hii.

“Matibabu mengi ya sasa ni ya kusaidia waathiriwa kupunguza kigugumizi wanapoongea, kwa mfano kwa kuzungumza polepole, kudhibiti kupumua kwao wakati huu, au kujifunza mazungumzo hatua kwa hatua kutoka silabi moja hadi maneno marefu na hatimaye sentensi ngumu,” aeleza Dkt Nzau.

Lakini huku haya yakijiri, wanasayansi ulimwenguni wanatafiti kuhusu mbinu za kutambua mapema na kutibu kigugumizi.

Kwa mfano, watafiti wamekuwa wakijitahidi kugundua jeni zinazosababisha hali hii na ambazo mara nyingi hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Wanasayansi wa taasisi ya kitaifa ya uziwi na matatizo mengine ya mawasiliano nchini Amerika-NIDCDC, wametambua utofauti katika jeni hizo ambazo zinasababisha kigugumizi miongoni mwa watu wengi ulimwenguni.

Watafiti aidha, wanafanya jitihada kusaidia wanapatholojia wa matamshi na lugha kutambua watoto ambao wana uwezakano mkubwa wa kuimarika kutokana na hali hii wanapoendelea kukua.

Vilevile, watafiti wanachambua mbinu za kutambua makundi ya watu wanaoonyesha tabia sawa za kugugumiza, ambazo huenda zinachochewa na suala moja.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wamsaka mmiliki wa lori lililosafirisha bangi

MUME KIGONGO: Ubora wa mbegu za kiume hufifia kadri umri...

T L