• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
SHINA LA UHAI: Wadau kikaoni wahimiza hatua zaidi kupigwa kuboresha afya

SHINA LA UHAI: Wadau kikaoni wahimiza hatua zaidi kupigwa kuboresha afya

NA PAULINE ONGAJI

MAKALA ya pili ya kongamano la kimataifa kuhusu afya ya umma barani (CPHIA 2022) yalifikia tamati jijini Kigali, Rwanda Desemba 15, 2022 huku mwito ukitolewa kwa serikali za Afrika kuongeza uwekezaji katika mifumo ya afya katika nchi zao.

Katika kongamano hilo lililoandaliwa na Muungano wa Afrika (AU) na kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani Afrika (Africa CDC), kati ya Desemba 13 na 15, lilihusisha zaidi ya washiriki 2,500 kutoka mataifa 90 barani Afrika na mbali, ikiwa ni pamoja na wakuu wa serikali, wanasayansi wa haiba ya juu, wawakilishi kutoka sekta ya kibinafsi, mashirika ya umma, na mashirika ya afya na ustawi ulimwenguni.

Ujumbe mkuu mwaka 2022 ulikuwa mataifa ya Afrika na washirika wa kimataifa kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za kiafya, kudhibitisha maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya, vile vile kuwezesha ufikiaji wa huduma ya afya kwa wote.

Sawa na kongamano la mwaka uliopita lililoandaliwa kupitia mtandaoni, pia wakati huu suala la mfumo mpya thabiti wa kiafya barani liliangaziwa, huku washikadau wakipaza sauti ya kuundwa kwa mtazamo mpya unaozipa nchi za Afrika uwezo wa kujiandaa kwa majanga ya kiafya katika siku zijazo.

“Mijadala hii inaonyesha tunachofanya ili kutimiza mfumo mpya wa afya barani na mazungumzo yetu yameonyesha kwamba tumepiga hatua kubwa tangu uzinduzi wa mkondo mpya wa afya miaka miwili iliyopita, lakini bado kuna mengi ya kufanya,” alisema Dkt Dkt Ahmed Ogwell Ouma, Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani Afrika (Africa CDC).

Kongamano hili ambalo ni la kwanza kuandaliwa moja kwa moja lilikuwa la kipekee, na taifa la Rwanda lililotwikwa jukumu la kutayarisha hafla hii, bila shaka ilikuwa imejiandaa vilivyo.Japo kulikuwa na udhaifu katika usafiri wa ndege, mpangilio wa mapokezi na mfumo wa kusafirisha wageni katika eneo la mikutano kwa siku hizo tatu za kongamano hili ulikuwa wa kipekee.

Lakini licha ya ufanisi na ushiriki mkubwa hasa ikizingatiwa kwamba huu ni mwaka wa pili tu wa kongamano hili, suala la mikutano kuandaliwa ili kujadili hali ya huduma ya afya hapa barani Afrika, sio geni.

Kwa mfano, kabla ya hapa kulikuwa na Azimio la Abuja (Abuja Declaration (2001), mkakati wa huduma ya Afrika barani (the Africa Health Strategy 2007-2015, 2016-2030) na mwito wa Addis Ababa wa kuchukua hatua kuhakikisha huduma ya afya kwa wote (Addis Ababa Call to Action on UHC 2019).

Katika Azimio la Abuja kwa mfano, viongozi wa nchi wanachama wa Muungano wa Afrika walipokutana jijjini Abuja, Nigeria, Aprili 2001, walikubaliana kutenga asilimia 15 ya bajeti ya serikali zao kwa afya. Hii ilikuwa kwa sababu rasilimali zaidi zilihitajika kuangazia changamoto za kiafya wakati huo kama vile virusi vya HIV na Ukimwi, maradhi ya Malaria na Kifua kikuu.

Lakini japo katika kipindi cha hivi majuzi baadhi ya mataifa ya Afrika yameongeza kiwango cha fedha zilizotengewa afya, ni nchi chache ambazo zimetimiza shabaha katika mwaka wowote ule.

Kufikia mwaka wa 2018 ni nchi mbili pekee zilizofikia shabaha hiyo.

Kwa sasa mataifa ya Afrika hutumia kati ya $8 na $129 kwa kila mtu kwa afya, ikilinganishwa na mataifa tajiri ambayo hutumia zaidi ya $4,000.

Hii ni kwa kutokana na masuala mbali mbali kama vile kiwango cha chini cha jumla ya pato la taifa (GDP) na kiwango cha chini cha ukusanyaji thabiti wa ushuru.

Kulingana na wataalam wa kiafya, kuna masuala kadha wa kadha ambayo yamesababisha sekta ya afya kupuuzwa barani inapowadia wakati wa kuitengea fedha.

“Afrika imekumbwa na changamoto ya uongozi mbaya, suala ambalo limetatiza tu sio sekta ya afya, bali maendeleo kwa ujumla. Aidha, umaskini umekuwa changamoto katika bara hili huku idadi ya watu ikiendelea kuongezeka,” aeleza Prof Francis Omaswa, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afya ulimwenguni barani Afrika (ACHEST).

“Pia, mataifa mengi ya Afrika, Kenya ikiwa miongoni mwao, hutegemea ufadhili kutoka nje ili kuendesha asilimia kubwa ya bajeti ya huduma za afya. Hii imesababisha mataifa mengi kushindwa kujitegemea katika sekta hii,” aeleza Prof Omaswa.

Mwaka 2022 ripoti kuhusu hali ya huduma nafuu ya afya kwa wote barani kwa jina State of Universal Health Coverage (UHC) in Africa Report, ilionyesha kwamba ni asilimia 48 pekee ya idadi ya watu barani wanapokea huduma za afya wanazohitaji.

Udadisi huo uliokusanywa kati ya Novemba 2020 na Machi 2021, uliashiria kwamba takriban huenda watu milioni 615 barani Afrika wasipokee huduma za afya.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la afya Duniani, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisistiza haja ya kuthibitisha mifumo ya afya kama njia ya maandalizi kupambana na majanga ya kiafya yajayo.

“Ikiwa mataifa ya Afrika yananuia kutimizi ndoto ya kuimarisha mfumo thabiti wa afya, basi yanapaswa kuendelea kuwekeza katika watu wake, vituo vya elimu na kuendelea kuhimili wanasayansi na wavumbuzi, miongoni mwa wataalamu wengine wa Kiafya,” Prof Senait Fisseha mwenyekiti mshiriki wa CPHIA na mkurugenzi wa miradi ya kimataifa katika hazina ya The Susan Thompson Buffet Foundation, alisema katika kongamano la mwaka 2022.

Kulingana na Prof Omaswa, ndoto hii itatimizwa tu iwapo suala la uongozi litaangaziwa.

“Aidha, suluhisho ni kuzungumza na viongozi wa nchi za Afrika na kuwarai kuwekeza zaidi sio tu katika afya, bali pia utafiti. Tatizo ni kwamba viongozi wengi barani huchukulia huduma ya afya kuwa mzigo, ilhali yaweza kuwa uwekezaji mkubwa.”

  • Tags

You can share this post!

Chelsea wapoteza alama muhimu katika EPL baada ya kuambulia...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Kansa ya ulimi hujitokezaje?

T L