• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 10:55 AM
Siri ya ufugaji nyuki ipo katika uongezeaji thamani

Siri ya ufugaji nyuki ipo katika uongezeaji thamani

NA SAMMY WAWERU

ASALI ni mojawapo ya mazao ya ufugaji yenye soko lenye ushindani mkuu.

Samuel Muhindi na binamu yake, Martin Mwangi wafugaji eneo la Karatina, Nyeri tangu waingilie ufugaji nyuki mwaka wa 2019 wanakiri ni biashara yenye mapato ya haraka. Ina faida.

“Asali haijawahi kukosa soko, na isitoshe, nchi hii hatujitoshelezi kiuzalishaji,” ndio kauli ya wafugaji hao.

Kenya huagiza karibu asilimia 80 ya asali kujaza pengo la upungufu, licha ya kuwa na raslimali za kutosha kuzalisha.

Hiyo ina maana kwamba tunazalisha asilimia 20 pekee. Huku kiwango cha uzalishaji kikisimamia metri tani 22 kwa mwaka, kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Kitaifa Kuhusu Ufugaji Nyuki, Ezra Owiti afisa wa mafunzo anasema mapato zaidi yapo kwenye uongezaji thamani.

“Siri katika ufugaji nyuki ipo kwa kusindika mazao,” Owiti aarifu.

Asali, Owiti anasema, inasindikwa (processed) kwa viungo kama vile chai, kahawa, ndimu, tangawizi, stroberi, lavender, blueberry, raspberry, hibiscus, miongoni mwa vingine.

Blossoms & Beehives, ni kampuni inayoongeza thamani zao hilo la ufugaji nyuki.

Ikiwa na tawi lake Nairobi Farmers Market, barabara inayounganisha jiji la Nairobi na Kiambu, Dorah James, mfanyakazi anaungama asali iliyoongezwa thamani ina mapato ya kuridhisha.

“Kwa kawaida, kilo moja ya asali iliyochujwa inachezea Sh700 na kipimo hichohicho kinapoungwa kinapanda hadi Sh1,000, Dorah aelezea. Kampuni hiyo ya kibinafsi inaendeleza ufugaji katika Kaunti ya Pokot Magharibi na Baringo.

Owiti anasema faida nyingine ya ufugaji nyuki ipo kwenye masega (honey comb). Wengi wakitupa bidhaa hiyo, mtaalamu huyu anasema ni dhahabu ambayo ikiongezwa thamani mfugaji atakuwa akila kwa kijiko na madaha kama Mfalme akiwa Kasri.

“Mishumaa, mafuta ya kujipodoa, sabuni, shampoo… ni kati ya bidhaa zinazotokana na masega, yanapogeuzwa kuwa nta (wax),” mdau huyu adokeza.

Ezra Owiti akionyesha nta ya asali inayotumika kutengeneza mseto wa bidhaa ikiwemo mishumaa. PICHA | SAMMY WAWERU

Anaambia Akilimali kwamba si lazima mfugaji awe na kiwanda, mashine au mitambo ya shughuli hiyo.

“Vifaa vya jikoni na vyombo, kama vile sufuria, vijiko, kichujio, karai na kuni vinatosha,” Owiti asema.

Afafanua: “Kwa kutumia sufuria mbili, moja yenye maji iwe chini kupata moto na nyingine masega, juu, kuyayeyusha kupata nta.”

Mabaki na nta yanatawanyika, nta ikihifadhiwa kwenye chumba chenye joto la kadri kupoa kwa muda wa saa 12. Nta inatumika kuunda mseto wa bidhaa. Taasisi ya Kitaifa Kuhusu Ufugaji Nyuki inatoa mafunzo hayo, Owiti akisema ada zinazotozwa ni nafuu mno.

“Tunahimiza wafugaji nyuki wajitokeze, tuwape mafunzo na kuwahamasisha mianya tele iliyopo kwa asali na bidhaa zinazotokana na nta,” Owiti ashauri.

  • Tags

You can share this post!

TUJIFUNZE THAMANI YA NYUKI: Wanachohitaji wafugaji ni...

UJASIRIAMALI: Ni Kamishna Msaidizi aliye pia muundaji wa...

T L