• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: CBC ikitekelezwa vizuri spoti itakua

TAHARIRI: CBC ikitekelezwa vizuri spoti itakua

KITENGO CHA UHARIRI

HUKU tukiwa katika mwaka wa tatu baada ya kuanza kutekelezwa kwa mtaala mpya wa elimu almaarufu CBC, wadau wakuu wanastahili kumakinika ili kutumia fursa itakayojitokeza kuhakikisha kuwa taifa hili linachipuza vipawa aula katika tasnia ya michezo.

Mtaala huu wa umilisi unashadidia uzamiaji wa mojawapo ya mikondo mitatu ya kitaaluma katika hatua ya amapema; Gredi ya 10 ambayo ni sawa na kidato cha pili katika mtaala wa 8-4-4.

Mwanafunzi anapoingia katika gredi hiyo, anatakiwa kuchagua mojawapo ya mikondo hiyo mitatu ya kitaaluma ambayo ni Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) likiwa kundi la kwanza, au masomo ya kisanaa yakiwemo ya lugha, ama ya ustawishaji talanta ambayo yanahusu ukuzaji vipaji kama vile muziki, kandanda, kwata na kadhalika.

Chambilecho wahenga udongo upatilize ungali mbichi au samaki mkunje angali mbichi, kuna umuhimu wa kufanikisha dhana hiyo iliyowaongoza wabunaji wa mtaala huu waliobaini kuwa urundikaji wa masomo mengi kwa mwanfunzi hadi kidato cha nne humchelewesha kuzamia kipawa chake alichojaaliwa na Maulana.

Mtaala wa sasa hasa umekuwa ukididimiza vipawa vya wanamichezo nchini maadamu aghalabu huwa wanahitajika kuendeleza vipawa hivyo sambamba na masomo mengine, hali inayotinga ukuaji wa vipaji vya wanafunzi; waama wahenga walisema mpanda farasi wawili hupasuka msamba.

Kwa mintaarafu hiyo, wanafunzi waliokirimiwa vipawa vya michezo wamekuwa wakiishia kuandama taaluma nyingine wasizozielewa vyema badala ya kukuza taaluma waipendayo wangali wachanga.

Kwa sababu hiyo, Kenya imekuwa na utaratibu mbovu wa kukuza vipawa vinavyoweza kuifaa zaidi kimataifa. Hasa katika fani ya kabumbu, tatizo hilo linadhihirika bayana kwani Kenya si taifa la kuogofya tena barani Afrika; huwa ‘linanyanyaswa’ na timu mahiri kama vile Nigeria, Misri, Algeria, Afrika Kusini, Mali, Ghana na kadhalika.

Tuna imani kuwa iwapo vipawa vitaanza kutambuliwa mapema na kukuzwa kitaaluma kama ilivyo katika mataifa mengine hasa ya bara Ulaya, Kenya itavuna pakubwa pale wanaspoti wake watakaposajiliwa na timu mahiri za ughaibuni na hivyo kujichumia pato zito maadamu katika mataifa hayo wachezaji huthamaniwa na kutunzwa inavyofaa.

You can share this post!

Mount afunga mabao matatu na kuongoza Chelsea kukomoa...

Chama pekee si kigezo cha kiongozi bora – Jungle

T L