• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Chama pekee si kigezo cha kiongozi bora – Jungle

Chama pekee si kigezo cha kiongozi bora – Jungle

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA ambao hawajajiandikisha wawe wapigakura wameshauriwa kufanya hivyo mara moja.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, amesema kwa majuma mawili yaliyopita, kumekuwa na idadi ndogo sana ya watu wanaojiandikisha kuchukua kura.

Uchunguzi uliofanywa na wadadisi wa kisiasa ni kwamba eneo la Thika na Kiambu kwa jumla, ni watu wachache sana ambao wamejitolea kujiandikisha.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita. mbunge huyo wa Thika amezuru maeneo tofauti kama Gatundu, Ruiru na Thika Mashariki ili kuwarai watu ambao wanasita kujiandikisha.

“Mwanasiasa yeyote anatambua uzuri wa wapigakura wanapojiandikisha kwa wingi. Kwa hivyo, nimechukua jukumu kuwahamasisha wananchi umuhimu wa kujihami na kadi ya kura,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema haya mjini Thika mnamo Ijumaa alipokuwa na msafara wa vijana kuelekea Gatundu Kaskazini kwa hamasisho la kuwahimiza wakazi kuchukua kura.

Alisema azma yake kwa sasa ni kujiandaa vilivyo kuwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Kiambu.

Bw Wainaina ametoa wito kwa wapigakura kutojali vyama vya kisiasa lakini wamjali mtu binafsi na kazi aliyotendea wananchi.

“Maswala ya vyama kwangu hayana umuhimu lakini mwananchi anastahili kumpima kiongozi kwa matendo aliyoyafanya,” alisema mbunge huyo.

Mbunge huyo alichaguliwa kwa tiketi ya kujitegemea yaani Independent mwaka wa 2017.

Alisema nchi hii inahitaji viongozi waliojitolea mhanga kuona ya kwamba wananchi wanapunguziwa mizigo ya madeni waliyobeba.

Alisema ni vyema kuwahamasisha vijana umuhimu wa kujiandikisha kwa wingi kwa sababu “kupiga kura ni kufanya maamuzi ya maisha yako.”

Mbunge huyo anajiandaa kumenyana na gavana wa sasa Dkt James Nyoro ambaye pia anaendesha kampei zake kwa kishindo akiangazia baadhi ya maendeleo aliyotekeleza kwa karibu miaka miwili sasa.

Gavana Nyoro anajivunia kuunda barabara sehemu tofauti za Kiambu, kuvuta umeme kuwafikia wakazi wa mashinani, kusaidia wakulima kupata mbolea na mbegu, na pia kuleta maji mashinani.

Aliyekuwa gavana wa hapo awali Bw William Kabogo, haijulikani kamili kama kweli anatamani kiti cha ugavana mnamo wakati ambapo anajaribu kujikita katika siasa za kitaifa.

Siku chache zilizopita Bw Kabogo alionekana katika msafara wa kinara wa ODM Raila Odinga alipozuru Kaunti ya Kiambu.

Siasa za Mlima Kenya zinazidi kugeuka kila kukicha huku viongozi wengi wakionekana kufuata maagizo ya Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

TAHARIRI: CBC ikitekelezwa vizuri spoti itakua

Man-City yakung’uta Brighton na kupaa hadi nafasi ya...

T L