• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
TAHARIRI: Uhifadhi mazingira usiwe ni siku moja

TAHARIRI: Uhifadhi mazingira usiwe ni siku moja

NA MHARIRI

MNAMO Jumamosi, Wakenya walijiunga na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.

Kama kawaida, viongozi na wananchi walijumuika katika maeneo tofauti kama mito, misitu, viwanja na chemichemi za maji kupanda miti na kufanya usafi.

Bila shaka, shughuli hizo zilifaa kabisa, kwani ziliwiana na kaulimbiu ya siku hiyo: Kuyajali mazingira.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa huwa tunaona juhudi hizo tu wakati siku hiyo inapowadia pekee, wala si nyakati zingine.

Swali kuu linaloibuka ni: Je, huwa tuko wapi siku hizo zingine wakati uchafuzi wa mazingira unapoendelea?Ni kinaya kuwa siku za kawaida, ni watu wachache sana huonekana kujali hali ya mazingira nchini.

Katika maeneo ya mijini, taka hutapakaa kila mahali. Wananchi huwa hawazingatii kanuni za msingi hata kuweka taka kwenye mapipa ama maeneo maalum yaliyotengwa. Kila aina ya uchafu hutupwa kwenye mito.

Maji ya mito mingi iliyopitia mijini huwa meusi kutokana na uchafu unaoelekezwa huko. Hakuna ambaye huonekana kujali.

Viwanda huelekeza maji yenye kemikali hatari kwenye mito hiyo bila kujali athari kwa viumbe wanaoishi humo ama watu ambao huyatumia maji hayo kwa shughuli za msingi kama kupikia na kuoga.

Kando na hayo, mito hiyo imegeuzwa maeneo ya kutupa miili ya watu wanaouawa.

Si mara moja tuneona miili ya binadamu iliyooza ikitolewa kutoka kwenye mito.

Cha kusikitisha ni kuwa, kuna watu ambao hutumia maji hayo kwa shughuli zao zote kwani huwa hawana mahali kwingine wanakoweza kutoa maji.

Misitu pia inakumbwa na hatari kama hiyo. Ukataji miti na uchomaji makaa umekuwa ukiendelea katika sehemu mbalimbali nchini, licha ya ufahamu wa baadhi ya wasimamizi wakuu serikalini.

Bila shaka, vitendo hivyo vimedhihirisha wazi huwa tunajidanganya eti tunahifadhi mazingira wakati tunapotokea kwa wingi na kujumuika siku hiyo.

Lazima serikali na wadau husika waanze hamasisho kali kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kukumbatia uhifadhi wa mazingira katika nyakati zote.

Hili litahakikisha wanachukulia uhifadhi kuwa miongoni mwa majukumu ya msingi wanayopaswa kutekeleza.

You can share this post!

Muungano wa kaunti umekufa

Mzozo kuhusu mpango wa kukabidhi Mumias Sugar usimamizi mpya