• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
TAHARIRI: Vurugu za kisiasa ni aibu, zikabiliwe

TAHARIRI: Vurugu za kisiasa ni aibu, zikabiliwe

KITENGO CHA UHARIRI

TUKIO la hapo Jumamosi ambapo msafara wa Naibu Rais William Ruto ulirushiwa mawe na kundi la vijana katika Kaunti ta Busia ni la aibu na hatari kwa ustawi wa taifa hili.

Msimu wa kampeni unapoanza kubisha hodi tukielekea kuandaa uchaguzi wa mwaka 2022, kutakuwa na misafara ya wanasiasa mbalimbali wakizuru pembe tofauti za nchi kunadi sera zao.

Katika kufanya hivi, kila mtu mwanasiasa atakuwa anajipigia debe.

Hii kwa kweli ni haki ya kidemokrasia ya kila Mkenya.

Hata hivyo, inashangaza kwamba hadi kufikia sasa, wapo wanasiasa ambao hawajakumbatia maana halisi ya demokrasia.

Wanadhani kwamba maeneo wanakotoka ni himaya zao ambazo zinafaa kulindwa dhidi ya ‘wageni.’

Mtazamo huu finyu wa mambo hufanya baadhi ya wanasiasa hawa kukodisha vijana na kuwalipa kwa azma ya kuwatumia kuvuruga mikutano ya kisiasa ya wapinzani wao.

Raila Odinga alipokuwa ziarani katika eneo la Mlima Kenya Mashariki, alikumbana na maeneo machache yaliyokuwa na vijana waliomzoma huku wakiimba nyimbo za kumsifu Naibu Rais.

Hili pia lililuwa kosa. Iwapo humpendi mwanasiasa fulani, basi hufai kuhudhuria mkutano wake na kuzua vurumai.

Salia nyumbani umsubiri mwanasiasa umpendaye atakapoandaa mkutano uhudhurie na umshangilie pamoja na kumpigia debe. Huu ndio utakuwa ukomavu katika siasa.

Ikumbukwe kwamba wanasiasa wa hadhi ya kuwania urais wana uungwaji mkubwa katika pembe mbalimbali wanakohisi ndizo ngome zao.

Iwapo mwanasiasa wa namna hii ataenda katika ngome ya mpinzani wake na azomwe au apurwe kwa mawe, basi tarajia kwamba tukio la namna hii litachochea ngome yake kufanya vivyo hivyo.

Ni msururu wa visa kama hivi ndio huchangia vurugu za kisiasa ama kabla ya kura au baada ya uchaguzi. Hatima kama iliyofika taifa mwaka wa 2007 na 2008 ilichochewa na matukio kama haya.

Kwa mintarafu niliyotaja, ni wajibu wa wanasiasa wetu kuanza kujenga kitiba cha ustaarabu wanapoendesha shughuli zao ili kuepuka kutumbukiza nchi katika machafuko ya kisiasa.

Wanasiasa wote wahubiri amani kwa wafuasi wao.

Aidha, idara ya polisi ina jukumu la kuhakikisha mazingira tulivu yanadumishwa katika hafla za kisiasa kwa kuwachukulia hatua wanasiasa wachochezi wanaochangia ghasia.

Tume ya Kitaifa ya Maadili izinduke na ianze kuchunguza visa vya vurugu na hatimaye kuwazuia wachochezi kushiriki katika uchaguzi.

You can share this post!

Raila yuko guu moja ndani Ikulu, Joho adai

Liverpool wadhalilisha Man-United kwenye EPL ugani Old...

T L