• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 9:50 AM
Raila yuko guu moja ndani Ikulu, Joho adai

Raila yuko guu moja ndani Ikulu, Joho adai

Na WACHIRA MWANGI

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa chama cha ODM amesema ishara zote zinaonyesha kuwa Raila Odinga atakuwa Rais wa tano wa Kenya.

Taifa litaandaa uchaguzi wake mnamo Agosti 2022, Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kustaafu baada ya kumaliza kipindi cha pili cha utawala wake.

“Nawashukuru wakazi wa Pwani kwa kumuunga mkono Raila katika chaguzi zote tatu ambazo zimepita. Kwa kuwa ishara zote sasa zinaonyesha kuwa atachukua uongozi wa nchi kwa nini msimpigie kura tena?” akasema Bw Joho akiwahutubia wakazi wa Likoni.

Gavana huyo ambaye aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Kisauni, akihutubia wakazi katika uwanja wa Mwahima mnamo Ijumaa, aliwataka wakazi wa Pwani wasichoke kuunga mkono Urais wa Bw Odinga.

Alimtaja waziri huyo mkuu wa zamani kama kiongozi mzalendo ambaye alipigania demokrasia nchini akisema ndiye mwenye maono ya kuendeleza miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais Kenyatta.

“Sote tujitokeze na wale ambao hawajajiandikisha kama wapigakura wafanye hivyo ndipo tumpigie Raila Odinga kura aingie ikulu mwaka ujao. Hapa kwetu karata yetu inafaa ianze kupangwa kuelekea uchaguzi wa 2027,” akaongeza.

Alifafanua kuwa alisalimu amri katika mbio za kuwania kiti cha urais kisha kumpisha Bw Odinga, akiamini kuwa ndiye kiongozi atakayeleta marekebisho zaidi yanayohitajika nchini kisha viongozi wengine wawanie wadhifa huo baada yake kuondoka mamlakani.

Viongozi wa kaunti hiyo walioandamana na Bw Joho akiwemo mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alisifu sera ya Bw Odinga ambapo vijana wasiokuwa na ajira watalipwa Sh6,000 kila mwezi akiingia mamlakani.

Alifananisha mfumo huo na ule ambapo wakongwe wamekuwa wakilipwa Sh2,000 kila mwezi na serikali ya Rais Kenyatta.

Bw Nassir alisema ana imani kuwa Bw Odinga ana nafasi nzuri ya kumbwaga Naibu Rais Dkt William Ruto mnamo 2022.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko naye alimshutumu Dkt Ruto kwa kuwahadaa vijana kwa kuwapa wilbaro badala ya kuwapa watoto wao kazi ilhali wanawe wamepewa kazi za ubalozi.

“Kwa nini Naibu Rais anawapa vijana wilbaro badala ya kuwaahidi nafasi za kazi. Mara hii tuna hakika Raila atakuwa Rais na atawapa hata watoto wetu vipakatalishi,” akasema Bi Mboko.

Viongozi hao wawili waliwahimizia raia ambao hawana kura wajisajili kwa wingi ili kumsaidia Bw Odinga kushinda Urais kwa kura nyingi mwaka 2022.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa makange ya kuku

TAHARIRI: Vurugu za kisiasa ni aibu, zikabiliwe

T L