• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
TALANTA YANGU: Mkariri na mwigizaji machachari

TALANTA YANGU: Mkariri na mwigizaji machachari

NA PATRICK KILAVUKA

UMACHACHARI wa mwigizaji wa mashairi Seline Khole, 9, mwanafunzi wa shule ya msingi ya Mother Margherita, Kawangware 56, kaunti ndogo ya Dagoretti North, umeonesha dalili za ndoto ya kipaji chake kufikiwa.

Anasema ukariri wa mashairi na uigizaji humpa raha sana.

Khole ni mtoto wa Bw Edwin Mulinda na Bi Sharon Habib.

Aliwasha mshumaa wa talanta yake akiwa Gredi ya Pili katika shule ya msingi ya Prudence Junior kwa uelekezi wa mwalimu Wanjiru.

Amepata fursa nyingine ya kujikuza baada ya kujiunga na anakosomea sasa mwaka huu na kutangamana na mwalimu Violet Nyabola ambaye amekigundua kipawa chake vyema na anakichochea kwa minajili ya kukikuza hata zaidi.

“Alijiunga moja kwa moja katika kikundi cha drama,” anasema mkufunzi Nyabola anayesimamia klabu ya drama shuleni.

Mkariri Khole ni mweledi wa kukariri, jasiri, mkakamavu na mchangamfu.

Mwanafunzi Seline Khole akionyesha miondoko yake ya kukariri shairi ‘The Sun’ katika siku ya kusaka talanta shuleni Mother Margherita, Kawangware 56. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Alishiriki katika mashindano ya tamasha za uigizaji ambazo ziliandaliwa kaunti ya Nakuru na kuibuka mshindi kwa kukariri shairi lenye mada ‘The Sun’.

Yeye hukariri mashairi kwa ustadi mno akionyesha weledi na huvutia kutokana na vile anavyotiririsha shairi lake.

Kwa sasa anajiandaa kwa tamasha za uigizaji za shule za msingi.Mwalimu Nyabola ndiye kioo chake katika mambo ya sanaa kutokana na tajriba yake.

Seline anapenda kula pizza kwa sababu ya utamu wake na ladha yake.

Angependa kuwa wakili ili kutetea masuala ya watoto na jamii.

Mambo ambayo anapenda kuyafanya wakati wake wa ziada ni kusoma hadithi za Yesu, kuimba na kutazama vibonzo.

Ushauri wake kwa wanafunzi wenzake ni kwamba watie bidii, wawajibike na wawe wavulana na wasichana wa kutenda mema na wadumishe nidhamu ya hali ya juu na pia wamche Mungu.

You can share this post!

Ombaomba: Jinsi walemavu bandia walivyonaswa mjini Thika

Zelensky ataja uvamizi wa Urusi kuwa ugaidi

T L