• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
TALANTA YANGU: Yeye ni kinanda cha uimbaji

TALANTA YANGU: Yeye ni kinanda cha uimbaji

NA PATRICK KILAVUKA

TALANTA ya mtoto ikichochewa mapema iwe ya masomo, sanaa au ya michezo inaweza kuwa kitovu cha kufaulu katika maisha yake kwani, vipaji vya watoto vitakuwa kitega uchumi siku za usoni.

Isitoshe, utumizi bora wa talanta za wanafunzi kujikuza kumechangia hata wengine kupata ufadhili wa masomo.

Kwa kutambua hayo, Cylnne Mukami,10, mwanafunzi wa Gredi ya nne katika shule ya msingi ya Junel, Kabete, Kaunti ya Kiambu ameazimia kuiandama ndoto yake ya kuwa mwimbaji siku za usoni.

Yeye ni mwanambee katika familia ya watoto wawili wa Bw Samuel Ngige na Bi Wanja Njuguna.

Alianza kuimba akiwa gredi ya kwanza katika shule ya msingi ya St Hellen Academy na kupitia kwa uimbaji, anafahamu fika kwamba atakuwa mhamasishaji wa jamii kupitia jumbe za nyimbo ambazo zinalenga uhimizaji na ukuzaji maadili.

Anakariri kwamba wakati huu wa likizo ndefu wanafunzi wanafaa kujipiga darubini vyema kubaini talanta zao.

Yeye hutumia wakati kama huu kufanya mazoezi ya kuimba kanisani ACK, Wangige na nyumbani kama njia ya kujinoa.

Shuleni anaelekezwa na mwalimu wake Josephine Akatu ambaye aligundua kipaji chake. Nyumbani amekumbatiwa na mama mzazi ambaye humhimiza kukuza talanta yake kwa kujihusisha kikamilifu katika uimbaji.

Mwalimu wake anasema chipukizi huyu ni mwimbaji aliyemtambua kutokana na ujasiri na ukakamavu wake katika kuimba mbele ya hadhira ya wanafunzi darasani na hafla za shule.

Isitoshe, aliamua kumpeleka kwa produsa wa muziki Shefady Muzikale ambaye alikiri kwamba, mwimbaji Mukami anayo sauti ya ninga ya uimbaji na anastahili kuelekezwa vyema.

“Baada ya kupata ushauri wa produsa, niliamua kumhusisha katika mkondo wa mazoezi shuleni na ameshika barabara ya kufikia ufanisi wa kipaji chake na hata kuwa kivutio cha wanagenzi wengine ambao wanapenda kuimba nyimbo,” anasema mwalimu Josephine.

Hata hivyo, sasa amepata mshawasha wa kutunga nyimbo zake, japo huimba nyimbo za wasanii kama Westlife – You Raise Me Up, utadhani ni chiriku!

Mbali na kuimba nyimbo kanisani na shule, yeye pia hupata fursa na kuimba katika sherehe zikiwemo harusi.

Mwimbaji ambaye ni kielelezo kwake ni Angelika Hale na uraibu wake ni kucheza michezo ya kwata ya watoto.

Isitoshe, yeye anahusudu sana kujikuza zaidi katika maadili mema akiwa mwanaskauti.

Ushauri wake kwa waimbaji chipukizi ni kwamba, wafanye mazoezi ya kila siku na watie bidii ya mchwa katika masomo na kukuza talanta zao.

Zaidi ya kutumia wakati wao wa likizo vyema anashauri kwamba wasisahau kuendelea kufanya marudio ya masomo ambayo huwa yanawatatiza.

You can share this post!

Kaunti zaidi ya 15 zakosa rekodi za ‘utajiri’ wake

SportPesa yapiga jeki timu za mashinani Murang’a

T L