• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tusikae kitako na kuanza kulalamika baadaye

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tusikae kitako na kuanza kulalamika baadaye

NA ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii kubwa na adhimu yenye ubora, heshima na ulwa ili kukumbushana na kuambizana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Kubwa zaidi ni kuwa tunakutana katika mwezi huu mtukufu wa ibada tukufu, ibada ya hija. Kabla ya kujitosa kwenye mada ya leo, kuihusu ibada hii ya hija, mojawapo ya nguzo ya dini yetu tukufu ya Kiislamu, hebu tukumbushane jambo.

Majuma kadha yaliyopita, katika ukumbi uu huu, tuliwaomba viongozi wetu wa dini kujitokeza kimasomaso na kutoa mwelekeo wa dini hasa katika kipindi hiki cha kampeni tukielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti tisa In Shaa Allah. Kusudio la ombi letu lilikuwa kuwa uongozi wan chi uendane na maslahi ya dini yetu.

Aidha, tulichukua nafasi hiyo kuwatakia kila la kheri wagombeaji wa nyadhfa mbali mbali za uongozi ambao kwamba ni waumini wa dini ya Kiislamu ili dini yetu ipate watetezi wa maslahi yetu kwa kudura zake Maulana. Tunakumbuka ni kwa namna gani mahitaji muhimu, au hata stakabadhi muhimu zimekuwa muhali kupatikana kwa waumini wa Kiislamu. Hata wakizipata ni baada ya kutokwa na damu na jasho.

In Shaa Allah tunazidi kuwatilia dua na kuwatakia kila la kheri wagombeaji na viongozi wetu wote Waislamu.

Ni kama kilio chetu hicho kilipata kusikika. Wiki za hivi karibuni tumewaona viongozi wetu wa Kiislamu wakihusika katika majopo, kamati, bodi na nyadhfa mbali mbali ambazo zipo katika mstari wa mbele kwenye kampeni za mwaka huu. Alhamdulillahi! Haifai kwetu sisi waumini wa Kiislamu kukaa tutwe na kuanza kulalama na kujuta tungalijua baadaye.

Vile vile, tumefurahi kuona kuwa viongozi wa Kiislamu wanaandaa vikao na kukutana na mirengo mbali mbali ambayo inagombea nyadhfa mbali mbali. Ni letu ombi na matumaini kuwa viongozi hawa wa dini yetu wanawasilisha maslahi na mahitaji ya dini yetu, yakiwemo maswala ya siku zetu kuu, ibada zetu, mazingira mwafaka ya ibada na maswala mengine kama hayo.

Isije ikawa kuwa baadhi ya viongozi wetu wanaandaa vikao na kualikana na wanasiasa kwa lengo la kuyaangazia maswala yao ya binafsi tu. La hasha! Ni makosa hayo. Na Mola Atuepushie hali kama hizo. Humu duniani sote tu wapita-njia.

Ikumbukwe kuwa hija ni mojawapo ya nguzo tano kuu za dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Ibada ya hija ya mwaka huu inafanyika kukiwa na utuvu na afueni angalau kuhusiana na janga la virusi vya Corona. Walau mwaka huu idadi ya mahujaji ni nafuu ikilinganishwa na ya miaka kama miwili hivi iliyopita. Alhamdulillahi tumshukuru mno Mola kwa unafuu huu.

Tuna imani kuwa ibada zijazo, kama hija ya mwaka kesho In Shaa Allah, itakuwa kubwa na yenye wingi wa mahujaji kuliko ya mwaka huu.

In Shaa Allah Mwenyezi Mungu Azitakabalia dua zetu na ibada zetu. Na pia mahujaji wetu wa mwaka huu ibada zao ziwe za kila kheri na wawe na safari njema kurejea makwao pasina majanga.

Ijumaa Mubarak!

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

DRC, Rwanda zakubali kusitisha uadui wao

Kura: Chebukati sasa akanusha madai ya Raila

T L