• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
DRC, Rwanda zakubali kusitisha uadui wao

DRC, Rwanda zakubali kusitisha uadui wao

NA ARNALDO VIEIRA

LUANDA, ANGOLA

JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda zimekubaliana kusitisha mapigano na uhasama baina yao, Rais wa Angola Joao Lourenco ametangaza.

Kufuatia mkutano jijini Luanda mnamo Jumatano, Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame pia walikubaliana kubuni kamati ya muda ya kusaidia kufanikisha mpango wa kupunguza taharuki.

Mnamo Jumanne wiki ijayo Angola pia itaandaa mkutano wa tume ya pamoja kati ya Rwanda na DRC, akasema Rais Lourenco, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kongamano la Kimataifa kuhusu Amani Eneo la Maziwa Makuu (ICGLR).

Kiongozi huyo alisema hayo katika wadhifa wake kama mpatanishi aliyeteuliwa na Muungano wa Afrika (AU) kuongoza mpango wa kukomesha mzozo kati ya Rwanda na DRC.

“Nina furaha kutangaza kwamba tumepata matokeo mazuri kwani tumekubaliana kuhusu kusitishwa mvutano wa kijeshi, miongoni mwa mikakati mingine ambayo imewasilishwa,” Rais Lourenco.

Uhasama umekuwa ukiendelea kati ya Rwanda na DRC kuhusu madai kuwa kila nchi inaunga mkono makundi tofauti ya waasi katika eneo la mashariki mwa DRC.

Mahusiano kati ya mataifa hayo mawili yalizorota zaidi baada ya DRC kuikashifu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23.

Rwanda ilikana madai hayo lakini baadaye ikaisuta DRC kwa kuunga mkono waasi wa FDLR ambao wanahujumu uthabiti wa serikali ya Kagame.

Mnamo Jumapili, Rais Tshisekedi alisema ana uhakika kwamba Rwanda inaunga mkono uasi nchini mwake baada ya kundi la M23 kurejelea mashambulio mashariki wa DRC, karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Awali, DRC ilipiga marufuku ndege za shirika la RwandAir kutua nchini humo.

Mchakato wa upatanisho, ulioongozwa na Rais Lourenco ulilenga kurejesha uhusiano na hali ya kuaminiana kati ya Rwanda na DRC.

“Angola ina tajriba pana katika masuala ya kusuluhisha uhasama na mapigano. Kwa hivyo, nina imani kwamba uhasama kati ya DRC na Rwanda utakomeshwa kupitia upatanisho unaosimamiwa na Rais Lourenco,” mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Macolino Taveres akaambia The EastAfrican.

You can share this post!

Man-Utd yamtega staa Antony na Sh7.2 bilioni

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tusikae kitako na kuanza kulalamika...

T L