• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 4:32 PM
UFUGAJI: Bidii yake inavyomvunia utamu wa asali Makueni

UFUGAJI: Bidii yake inavyomvunia utamu wa asali Makueni

NA LABAAN SHABAAN

ZIARA aliyoifanya kwa binamu yake akiwa likizoni mnamo 2017, ilimpatia fursa ya kupata mizinga mitatu ya kiasili na kuchochea kuasisiwa kwa kampuni ya Bee Love Apiaries.

Baada ya miaka mitano, mwasisi wa taasisi hii ni mtalaamu anayetambulika katika uzalishaji wa asali. Jonesmus Wambua ni mkurugenzi wa kampuni ya ufugaji wa nyuki maarufu Bee Love Apiaries eneo la Makindu lililoko Kaunti ya Makueni.

Wambua huandaa warsha za kuelimisha wafugaji wengine sehemu tofauti nchini.

“Tunashughulikia wakulima hadi nje ya Makueni kama vile maeneo ya Pwani, Mlima Kenya, Magharibi na pia Bonde la Ufa. Ufugaji nyuki ni msingi wa maisha endelevu kupitia kilimo,” Wambua anaeleza.

Miongoni mwa huduma ambazo Bee Love Apiaries hutoa ni kutambua sehemu mwafaka za kunasa nyuki, kukita mizinga, kusimamia miradi ya nyuki, na kununua asali kutoka kwa wafugaji aliowafunza.

“Chuoni nilisomea sayansi ya takwimu lakini kwa sababu ya shauku yangu ya kilimo nikazamia ufugaji nyuki. Nashauri wengine wajiunge nami kwa sababu bila nyuki hakutakuwa na uchavushaji hivyo hakutakuwa na chakula duniani,” Wambua anaambia Akilimali.

Safari yake Jonesmus ilianza kwa kukita mizinga ya kiasili kufuga nyuki.

Chaguo hili lilikuwa na changamoto wakati wa ukaguzi na kurina asali, kiwango cha chini cha ubora wa asali na pia kutodumu muda mrefu.

“Siku hizi tunashauri wafugaji nyuki kukumbatia mitindo ya kisasa kwa sababu mitindo ya kiasili huhatarisha maisha ya nyuki na kuharibu asali wakati wa kurina kutumia moto. Vifaa vya kisasa huongeza thamani ya asali na hutunza nyuki,” anaarifu.

Bee Love Apiaries hupendelea mizinga aina ya Langstroth yenye ubora usioathiriwa na maadui kama vile nyegere, nyigu, buibui na siafu ambao hula asali.

Kwa desturi, wafanyakazi wa kampuni hii huvuna kilo 10 katika kila mzinga baada ya kati ya miezi sita na mwaka mmoja. Wambua ameajiri wafanyakazi watano. Katika kipindi hiki, mwanatakwimu huyu husindika tani moja ya asali aliyozalisha pamoja na ile ambayo ananunua kutoka kwa wafugaji wengine wa nyuki.

“Sisi hununua asali isiyosindikwa kutoka kwa wakulima. Tulichukua mkondo wa kufunza wafugaji na kununua asali yao kwa sababu ya kuondoa madalali wanaowapunja wazalishaji asali,” Wambua anasema.

Wanunuzi hupata asali kwa Sh1 kwa kila gramu; kwa hivyo kilo moja ya asali ni Sh1,000 na huuzwa sehemu zote Kenya ambapo muuzaji huyu pia hutoa huduma ya kuwasafirishia wateja. Kadhalika Jonesmus huuza mizinga kwa wazalishaji asali na kuandamana nayo huwapa bila malipo daftari aliyotengeneza ya kuweka rekodi ya uzalishaji wa kila mzinga na mazingira.

“Kalamu fupi zaidi ni bora kuliko kumbukizi refu zaidi. Ukiwa na mizinga 1000, huwezi kukumbuka yote kwa hivyo ni lazima uweke rekodi ya aina ya miti, kiwango cha maua na misimu ya kuchanua,” Wambua anaeleza umuhimu wa kisomo chake katika kazi hii.

Kila mwaka Bee Love Apiaries huandaa warsha nne kufunza mbinu za kuzalisha asali na hugharimu Sh3,000 kwa kila mkulima kupokea mafunzo kikamilifu. Wenye nia ya kuanza huuziwa mzinga kwa Sh5,500 na kuwekewa bila malipo.

Wambua anaambia Akilimali kuwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi na msukosuko wa uchumi umeathiri sana biashara yake na anaomba serikali ya Kaunti ya Makueni kusaidia makundi kuanza biashara hii ili asaidie kuimarisha.

  • Tags

You can share this post!

Wataalam wakongamana JKUAT kubadilishana mawazo kuhusu...

UJASIRIAMALI: Karani anayekuza mboga za kienyeji

T L