• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
UJASIRIAMALI: DJ anayekupa burudani aali akijihakikishia kipato kizuri kwa kuwapokeza wengine ujuzi

UJASIRIAMALI: DJ anayekupa burudani aali akijihakikishia kipato kizuri kwa kuwapokeza wengine ujuzi

NA MARGARET MAINA

MIAKA ya nyuma, kazi ya u-DJ yaani deejaying mara nyingi haikuzingatiwa lakini baada ya muda, madeejay wamethibitisha kuwa sanaa hii inafaa kupewa fursa.

Stan Njenga Kinyanjui anayejulikana kama DJ Stan, amefanya mageuzi katika uchezaji muziki mitaani na sasa ameanza kuwafundisha vijana ili nao wawe stadi na magwiji katika tasnia ya burudani.

Kwa mtaji wa Sh650,000, Stan ameanzisha akademia ya Deejay jijini Nakuru, inayotoa kozi fupi na ndefu za deejaying.

“Tunatoza Sh30,000 kwa muda wa miezi miwili ambayo inashughulikia mambo ya msingi tu wakati kwa kozi ndefu za muda wa miezi 5 tunatoza Sh50,000 ambayo inashughulikia vitengo 5 vya u-DJ.”

“Ukweli kwamba vijana wengi wanaotamani kuwa DJ wamekuwa wakiniomba niwafunze, ulinipa wazo hili. Nilikuwa nikiwafunza baadhi ya watu kutoka nyumbani kwangu, lakini niliona itakuwa ni jambo zuri kwangu kufanya hivyo kwa weledi,” anasema.

Ikizingatiwa kuwa baadhi ya ma-DJ wamepata nafasi ndogo ya kupata ujuzi wa taaluma ya deejaying kutoka chuo kinachotambulika, Dj Stan anaamini kuwa shule yake itaweza kuwasaidia vijana wengi ili kuziba pengo lililoko.

“Sekta ya deejaying ni pana sana. Hii ni kwa sababu kuna aina nyingi za ma-DJ. Ma-DJ hawa wote na wanachofanya kwenye tasnia ya burudani wana majukumu yao ambayo yanawapa sababu za kuwepo kwenye tasnia hiyo,” anasema.

Alianzisha shule yake hiyo mwaka wa 2017, ikianza na wanafunzi 10 na hadi sasa imetoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 70.

Programu hizo huendeshwa kwa mtindo wa kitaaluma, huku chemsha bongo, mitihani ya mwisho na vyeti vikitolewa kwa wale ambao wamemaliza kozi hiyo kwa mafanikio.

Dj Stan alipenda muziki tangu utotoni.

“Nilikuwa nikiimba kanisani na kucheza ala,” anasema.

Baadaye alisoma Deejaying kama kozi katika System Unit Dj Academy.

Dj Stan anasema kuwa chuo chake kinakusudia kuongeza wateja na anawahimiza wasichana na wanawake zaidi kujaribu, akisema kuwa imekuwa kawaida kazi hiyo kutambulika kama tasnia inayotawaliwa na wanaume.

Baadhi ya wanafunzi wa DJ Stan. PICHA | MARGARET MAINA

Bila shaka wacheza diski (DJs) ni miongoni mwa watetezi wakuu na mabalozi wa muziki wa Kenya na wana umuhimu mkubwa kwa vilabu vyoyote vinavyotaka kutambulika kwa kutoa burudani safi kwa wateja.

Mtu akitilia maanani somo la u-DJ, Dj Stan anasema kuwa deejaying inaweza kuwa kazi ambayo kila Dj anayependa anaweza kujikimu kimaisha kwa urahisi.

“Ninapoangalia jinsi baadhi ya vijana wanavyofanya vyema zaidi kutokana na ujuzi wa kimsingi wa deejaying niliowapa, ninapata motisha kufanya vizuri zaidi katika kuwafunza wengine ili wakue kitaaluma,” anaeleza.

“Kinyume na kinachoaminika huko nje, kujifunza kuwa DJ sio rahisi na mafanikio hayaji mara moja. Ni safari inayoweza ikachukua muda mwingi hivyo jitihada, bidii, na kutenga wakati ni muhimu. Si vigumu kuanza. Lakini ni vigumu kujitokeza na kuwa na upekee,” anamalizia.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya 5 milioni wameathiriwa na njaa, ripoti yabainisha

Kongamano kuhusu ajenda ya afya kuandaliwa jijini Kigali...

T L