• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
UJASIRIAMALI: Kuchelewa kuwasili kwa zawadi yake Siku ya Wapendanao kuliamsha ari yake kujitosa kwa biashara ya maua

UJASIRIAMALI: Kuchelewa kuwasili kwa zawadi yake Siku ya Wapendanao kuliamsha ari yake kujitosa kwa biashara ya maua

NA MAGDALENE WANJA

BI Marion Wambui alikuwa katika kipindi cha mwanzo katika uhusiano wake na mumewe, na kama ilivyo kawaida kila mmoja wao alitaka kumfurahisha mwenzake kwa zawadi.

Siku ya wanamapenzi “Valentine’s Day” ya mwaka 2018, mpenzi wake alinunua maua kutoka kwa duka moja mtandaoni ambayo alitaka yafikishwe kazini kwa Bi Wambui.

Bi Wambui hakujua mpango wa mpenzi wake, na ilipofika saa za kufunga kazi, aliondoka , ila zawadi yake ya maua haikuwa imefika.

Alipoenda kukutana na mpenzi wake baadaye, alitaka kujua kama alipokea zawadi yake, ila Bi Wambui alishangaa kwani hakutarajia zawadi yoyote.

“Zawadi hiyo ililetwa siku iliyofuatia ambapo tayari maua yalikuwa yameanza kunyauka na hayakupendeza,” asikitika Bi Wambui.

Kwa kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kupokea maua alifurahia sana na alitaka kujua zaidi kuhusu biashara hii ya maua.

“Nilianza kuvutiwa sana na biashara ile na niliamua kuifanya katika muda wangu wa ziada,” anasema Bi Wambui.

Kwa kuwa hakuwa na ujuzi mwingi katika sekta hiyo, alifanya utafiti na akagundua kwamba, kuna shule ambazo angeenda huko kusomea taaluma hiyo.

Alijiunga na chuo cha Accol Floral Design Training Center. Hii ilifuatiwa na kozi nyingine katika chuo cha New Media School ambapo alipata ujuzi wa kutosha kuendesha biashara yake.

Bi Marion Wambui ni muuzaji wa maua. PICHA | MAGDALENE WANJA

Kutokana na kazi yake ya hapo awali, alikuwa ametenga Sh50,000 ambazo alizitumia kuanzisha biashara yake ya maua.

“Nilihisi kwamba nilikuwa na ujuzi wa kutosha na nilielewa jinsi ya kupata faida katika sekta hii,” akaongeza Bi Wambui.

Aina mbalimbali za maua huuzwa kwa bei tofauti ambayo huanzia Sh1,000.

Wakati wa janga la Covid-19, biashara yake ilifanya vyema zaidi na aliweza kuhamia kwenye duka kubwa ili kumwezesha kuhudumia idadi kubwa ya wateja.

Bi Marion Wambui ni muuzaji wa maua. PICHA | MAGDALENE WANJA

Kufikia sasa, biashara yake inawahudumia kati ya wateja 400 na 600 kila mwezi.

“Nina uhusiano wa karibu na wateja wangu, jambo ambalo huniwezesha kuelewa aina ya maua ambayo wanahitaji, kwani mahitaji ya wateja hutofautiana,” anaeleza Bi Wambui.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ni kosa kubwa kuwasawiri waliounga mkono...

Ni wikendi ya kisasi EPL

T L