• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
UJASIRIAMALI: Sanaa ya kuchonga glasi inavyowajenga

UJASIRIAMALI: Sanaa ya kuchonga glasi inavyowajenga

NA MARGARET MAINA

AKIWA kijana, David Karitha alikuwa akimtazama mjomba wake akitengeneza vitu vya asili vya kupendeza kutoka kwa glasi.

Hii ilikuza hamu yake ya kujifunza na mnamo 2006, alianza kuchora vioo lakini kama burudani tu wakati akiboresha ufundi wake. Mnamo 2008, aliuza kipande chake cha kwanza, bakuli ya saladi kwa Sh2,500.

Hadi sasa, plastiki, mbao, kioo, na ngozi zinaweza kubadilishwa ili kuangazia uandishi na katika baadhi ya matukio, picha za maelezo mazuri. David na mkewe Ruth Karimi, wamekuwa wakichora miundo na maneno kwenye glasi kwa miaka 11, wakichukua glasi iliyochakaa na kuifanya kuwa bidhaa ya kifahari.

Wakiwa na mtaji wa Sh70,000 waliokopa kutoka kwa benki, wawili hao walianzisha Elegance Simplified mwaka wa 2017.

Mtaji huo ulitumika kununua mashine za kuchonga, zana na malighafi.

“Elegance Simplified inahusika na sanaa ya kioo. Tunachonga bidhaa tofauti za glasi kutoka kwa glasi za kunywea, kuning’inia ukutani, milango ya vioo na sehemu za ukuta. Zaidi ya hayo tunatengeneza mabango ambayo yanaweza kutumika kama ishara za shukrani, tuzo na sifa,” anasema David na kuongeza kuwa wanatumia glasi iliyosindikwa.

Uchoraji wa glasi ni njia nzuri na ya kifahari ya kuunda muundo wa picha kwenye kipande laini cha glasi. Ni ya kudumu na haitatoka kamwe.

Vioo vilivyochongwa vimekuwa maarufu sana siku hizi, na unaona kila mahali katika mikahawa ya hali ya juu, hoteli, benki, kumbi za sinema na majumba.

“Chupa ya mvinyo inaweza kutumika kutengeneza glasi ya kunywa, au bakuli ya saladi ya ukubwa wa wastani au vishikio vya balbu na mengine mengi,” asema.

Ruth alisomea Usimamizi wa Biashara huku David akiwa bwana wa ufundi, wawili hao wanapata baadhi ya glasi kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani au kutoka nje ya nchi huku kwa chupa zilizosindikwa wanapata kutoka kwa wakusanyaji vioo.

“Tunaanza kwa kutambua bidhaa tunazotaka kutengeneza. Kisha tunachagua chupa za kufanya kazi. Tunazisafisha, kuzikata na kuzing’arisha. Zile za kuchonga, tutafanya kazi kwenye miundo au kazi za sanaa na baada ya kukamilika, tunazifunga na kuzitayarisha kuuza.”

David anasema kwamba kwa kazi nyingi za sanaa, yeye hutumia ufuatiliaji wa picha ili uwe na usahihi na Ruth anaongeza shanga za kifahari kwenye vipini vya kioo.

Elegance Simplified inatumia mbinu za uuzaji kulingana na wateja wao na hutumia majukwaa anuwai kufikia wateja wao.

Wanaonyesha kazi yao katika duka lao lililopo The Waterfront, Karen. Mbali na kutumia majukwaa yao ya mitandao ya kijamii kuuza bidhaa zao, wawili hao hushiriki katika masoko mbalimbali ya ufundi na pia kuuza vipande vyao kwa wauzaji wengine.
Wateja wao ni kama vile Ahadi Kenya Trust, The Nairobi Japanese School, Full of Africa Safaris, Top Guide Safaris in Tanzania, Windsor Golf Club, na wengine wengi.

“Tuna zaidi ya bidhaa 25, bei zinaweza kutofautiana kulingana na saizi, mchoro na idadi ya bidhaa zilizoagizwa. Kiwango cha chini tunachotoza kwa kipande ni Sh1,000 huku kipande cha bei ghali zaidi kinaweza kufikia Sh250,000.”

Kwa siku, wanaweza kuchonga kati ya seti 8 hadi 10, ambapo seti ina vipande 6.

Mbali na biashara hiyo kuwa tegemeo kubwa kwa wanandoa hao, Elegance Simplified imetengeneza ajira kwa kuwashirikisha wachongaji wengine, wasafishaji na kazi nyingine za kimkataba.

Haijawa rahisi kwa wawili hao bila changamoto zao.

“Biashara yetu ni ya msimu, kwa hivyo tunapaswa kutafuta soko sahihi la bidhaa zetu. Kwa wateja wetu wa ng’ambo, tunapaswa kukabiliana na gharama kubwa ya usafirishaji nje ya nchi.”

Licha ya hayo, David anaamini kwamba biashara yake ambayo ilikuja kutokana na mapenzi ya sanaa ya kioo, imechangia pakubwa sio tu kukuza uchumi wa Kenya, bali pia kuhifadhi mazingira.

Elegance Simplified unashughulikia kuingia kwenye masoko ya kimataifa. Hivi majuzi walitia saini mkataba na wakala wa mfumo ikolojia wa E-commerce ili kuuza bidhaa hizo kwa masoko ya Marekani na Kanada.

Lengo lao ikiwa ni kupanua wigo wa bidhaa na kuongeza sehemu yao ya soko kwa kuhakikisha mwendelezo wa kubaki muhimu katika soko linaloendelea na kuvutia wateja wao na jamii kwa ujumla. Hii anasema itakuwa muhimu kwa upanuzi wa kampuni.

“Tunapanga kuanzisha chuo cha sanaa ya kuchonga vio kwa ajili ya vijana katika siku za usoni,” anamalizia.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Kifaa cha kunasa wadudu waharibifu wa matunda...

Ebwali, Highway katika makundi makali Arusha

T L