• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
MITAMBO: Kifaa cha kunasa wadudu waharibifu wa matunda mitini

MITAMBO: Kifaa cha kunasa wadudu waharibifu wa matunda mitini

NA RICHARD MAOSI

WANASAYANSI wamekuwa wakijikuna vichwa, wengi wao wakitaka hatua ya dharura kuchukuliwa ili kukabiliana na wadudu wanaoshambulia mavuno yangali shambani hususan maembe, machungwa, mipapai na matikitimaji.

Hali ilizidi kuwa mbaya pale wingu la nzige, viwavi jeshi na wadudu wa fruit flies, waliposhambulia mashamba, jambo ambalo liliwafanya baadhi ya wakulima kutumia nyenzo za kiasili kuwadhibiti kwa kupulizia dawa zenye kemikali.

“Kwa upande mwingine, ikumbukwe kuwa matumizi ya kemikali yanaweza kudhuru afya ya binadamu, huenda kutokana na kutofahamu maelezo ya kimatumizi,” anasema Agnes Mbithe mkulima wa matunda kutoka eneo la Nziu katika Kaunti ya Makueni.

Mbithe ambaye vilevile amawahi kuhudumu katika Taasisi ya Kilimo na Ufugaji (KALRO), ameamua kutumia ujuzi wake wa zaidi ya miaka 30 kuendesha kilimo chenye tija.

Anaongezea kuwa endapo madawa haya yatatumika kwa muda mrefu kukuza matunda yanaweza kusababisha maradhi ya saratani na hata yale ya ngozi.

Alifichulia Akilimali kuwa dawa za kemikali zinapotumika huathiri mazingira kwa kuwaua wadudu wenye manufaa ya kulainisha mchanga wanaopatikana kwenye udongo.

Anasema ndio maana wataalam wamevumbua kifaa cha fruit fly bait ambacho mara nyingi huchukua rangi ya manjano, ambapo kifaa chenyewe hutundikwa juu ya shina la mti na kuachwa hapo na mkulima.

Lengo kuu likiwa ni kuwaepushia wakulima gharama ya kununua dawa zenye kemikali, pia kukuza matunda yenye afya na virutubishi asilia vyenye manufaa katika mwili wa binadamu.

Isitoshe, mtambo wenyewe umepatiwa jina la mtego wa wadudu wa matunda ambao unaweza kuwanata pindi wanapoingia ndani ya kifaa hiki.

Mbithe anasema kuwa matumizi ya kifaa hiki ni mepesi, ndio maana anawashauri wakulima mashinani kukumbatia mfumo huu ambao unaweza kuwafaidi wanaokuza matunda kwa matumizi ya nyumbani ama kwa ajili ya kuuza sokoni.

Ikumbukwe kuwa wadudu wa fruit flies husababisha hasara kubwa kwa wakulima wa matunda kwani mara nyingi wamekuwa wakivamia sehemu laini za matunda na kuyatafuna, na kuyaacha yakioza shambani.

Hivyo basi, ili mkulima amudu kuyakinga matunda yake dhidi ya wadudu hawa anastahili kuweka mikakati ya mapema ili kuzuia hasara kubwa ambayo anaweza akaikadiria wakati wa kuvuna.

Kifaa cha fruit fly bait huchukua umbo la kasuku ya mviringo ambacho huwa na rangi ya manjano , ambayo imewekwa mahususi ili kuwavutia wadudu.

Kifaa cha Fruit Fly bait ambacho hutumika kuwaangamiza wadudu ambao hushambulia matunda. PICHA | RICHARD MAOSI

Kulingana na utafiti imebainika kuwa ni rahisi kwa wadudu kama vile vipepeo kuvutiwa na rangi ya manjano ambayo mara nyingi hupendeza machoni.

Kifaa hiki vilevile huwa kimewekewa matundu, sehemu ambayo fruit flies hutumia kupenyeza na kuingia ndani ya fruit fly bait.

Mara tu wadudu wanapojitosa ndani ya kifaa hiki hawawezi kuondoka hata wakipambana namna gani na baadae wao huzama ndani ya kitu kiowevu (liquid) ambayo huwa ndani ya kifaa chenyewe.

Mbithe ambaye pia amewahi kufanya kazi katika mashirika ya kuchunguza ubora wa udongo, ikiwa ni pamoja na kuangazia maswala muhimu ya ikolojia anasema kuwa ni kifaa ambacho angalau kimekuwa kikimpunguzia gharama ya kukuza matunda, hasa inapokuja katika swala la kusaka dawa ya kukabiliana na viwavi jeshi.

Anaongezea kuwa sehemu nyingi za Ukambani hukuza idadi kubwa ya matunda kuanzia maembe hadi machungwa ambapo changamoto kubwa imekuwa ni namna ya kukabiliana na maradhi yanayosababishwa na wadudu.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Nafaka mpya zatoa jibu la kudorora kwa mazao

UJASIRIAMALI: Sanaa ya kuchonga glasi inavyowajenga

T L