• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Uvumbuzi: Trekta inayotumika kwenye mashamba madogo

Uvumbuzi: Trekta inayotumika kwenye mashamba madogo

NA SAMMY WAWERU

TEKNOLOJIA na mifumo ya kisasa kuendeleza kilimo ni miongoni mwa mbinu zinazotajwa kuchangia pakubwa ongezeko la uzalishaji wa chakula nchini.

Kando na kurahisisha shughuli ya zaraa, shirika lisilo la kiserikali la Heifer International linasema teknolojia inavutia vijana kushiriki.

Kulingana na kampuni hiyo yenye tawi lake nchini kupiga jeki wakulima, mifumo ya kisasa inashabikiwa na vijana ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipuuza kushiriki kilimo.

“Licha ya kuwa tunalalamikia idadi ya chini ya vijana kuwa kwenye kilimo, tunapaswa kuwateka kwenye mtandao wa uzalishaji chakula kupitia teknolojia za kisasa na vumbuzi,” asema George Odhiambo, afisa kutoka shirika hilo.

Nyabon Enterprises Ltd, kampuni inayounda mashine za kilimo imeibuka na trekta inayotumika kwenye mashamba madogo.

Meneja wa Mauzo na Soko, Vincent Odhiambo anasema mashine yenyewe inalenga wakulima wa mashamba madogo.

Meneja wa Mauzo na Soko Nyabon Enterprises Ltd, Vincent Odhiambo akionyesha jinsi trekta ndogo na ya kisasa inavyolima katika hafla ya Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara na Kilimo (ASK) Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Ikiwa na injini ya silinda 4, maarufu kama mini tractor ina nguvu za 27HP.

“Inavuta majembe mawili (sheer plough disc) na kulima ekari tano kwa siku,” Vincent adokeza.

Ongezeko la idadi ya watu nchini ikichangia kiwango cha mashamba kupungua, afisa huyo aidha anasisitiza haja ya kukumbatia mifumo na teknolojia za kisasa kuafikia malisho.

“Injini yake ni ya mafuta ya dizeli, na kwa kila eka inatumia lita tano pekee,” aelezea, akiongeza kuwa trekta hiyo ya kisasa pia inaweza kutumika kusafirisha mizigo.

“Mbinu za kitambo kuendeleza kilimo ni ghali na zinazochosha. Ili kuteka vijana washiriki kilimo; teknolojia, mifumo na mashine za kisasa zitawavutia na kama taifa tutafanikiwa kukabili kero ya njaa na upungufu wa chakula,” Vincent afafanua.

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu Kisumu inauza trekta hiyo Sh1.6 milioni, vifaa kuiunganisha vikiagizwa kutoka India.

Wadauhusika wakiendelea kuhamasisha wakulima kukumbatia teknolojia za kileo, Nyabon Enterprises ilitumia jukwaa la Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara na Kilimo Nairobi, mwaka huu kuvumisha trekta hiyo.

Yaliandaliwa na Muungano wa Kilimo Nchini (ASK), mwenyekiti tawi la Nairobi Joseph Mugo akitaja bunifu na teknolojia za kisasa kuboresha kilimo kama mojawapo ya mbinu kuokoa mazao.

  • Tags

You can share this post!

Klabu 18 kukutana na waziri Namwamba

Mto Ewaso Nyiro waendelea kukauka athari hasi za mabadiliko...

T L