• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
NGUVU ZA HOJA: Hili swali ni gumu na vilevile rahisi, Je hii lugha ya Kiswahili inalipa?

NGUVU ZA HOJA: Hili swali ni gumu na vilevile rahisi, Je hii lugha ya Kiswahili inalipa?

NA PROF IRIBE MWANGI

MWANAFUNZI wangu wa uzamivu katika chuo Kikuu cha Nairobi kwa jina Nicholus Makanji aliniuliza swali. Swali lililonifikirisha sana. Swali nililoshindwa kulijibu.

Si kwa sababu ya ugumu wake, bali kwa sababu ya wingi wa majibu niliyotaka kumpa kwa wakati mmoja nisiweze kubainisha lipi kubwa kuliko jingine. Swali lenyewe lilikuwa: Je, Kiswahili kinalipa?

Ni swali nililoliona rahisi lakini likawa gumu kutoa kauli ya moja kwa moja. Hivyo basi nitamjibu kupitia ukurasa huu ili kuwafaa na wengine. Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi nchini Kenya. Kuna nafasi nyingi sana za kazi za Kiswahili kutokana na hadhi yake hiyo.

Kiswahili kinafunzwa na kutumiwa katika kufunzia shuleni na hata vyuoni. Walimu wanahitajika ili kutekeleza hili. Kiswahili basi kinawapa vijana ajira. Vijana wengine wengi wameajiriwa katika sekta mbalimbali kutokana na ujuzi wa Kiswahili. Yapo mashirika yaliyowaajiri wengi kama watafsiri na hata wakalimani. Wapo vijana walioajiriwa kushughulikia mitandao inayotaka kuwafikia wateja wake kupitia kwa Kiswahili. Vijana hawa wanabuni mitambo yenye Kiswahili kama lugha mojawapo.

Wapo wahariri wengi ambao wameajiriwa kote ulimwenguni katika mashirika yanayochapisha vitabu kuhusu na katika Kiswahili.

Mpenzi wa Kiswahili ana nafasi ya kuzuru nchi nyingi kama mkalimani. Kongamano linapotokea, hukuza uchumi wa nchi husika. Watalii huzuru nchi na kuhudumiwa na wahudumu mbalimbali. Biashara ya hoteli hupata kazi kwa wingi. Kwa kuelewa Kiswahili, inawezekana kutangamana na watu wengi na hivyo kuweza kufanya kazi sehemu nyingi Afrika Mashariki na hata ulimwenguni.

Jibu langu kwake basi ni: Ikiwa haya si malipo, je, tuyaite nini?

  • Tags

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya...

Boga ajiandaa kupinga Achani mahakamani

T L