• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Kayole South (CHAKIKA)

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Kayole South (CHAKIKA)

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika shule ya upili ya Kayole South jijini Nairobi (CHAKIKA), kilizinduliwa 2021 na walimu Shadrack Igunza na Julida Kemuma.

Vilevile, kinahimiliwa na walimu wote katika Idara ya Kiswahili wakiwemo Bi Jecinta Bosibori, Bw Duncan Waweru, Bw Stanley Ngugi na Bi Irene Akinyi. Mbali na wawakilishi wa kila kidato, wanafunzi wanaoongoza chama kwa sasa ni Floyd Ogola (Mwenyekiti) na Carren Waceke (Katibu).

Chama kina vitengo vinne vikuu – Ushairi, Uanahabari, Uigizaji na Uandishi. Wanachama hujigawa kwenye vitengo hivi ili kujadili masuala yanayowahusu wanapokutana kila Jumatano.

Waigizaji wanaoongozwa na Monica Adhiambo na Louis Mwangi hutumbuiza wageni nyakati za hafla muhimu shuleni. Mashairi nayo hutungwa na kukaririwa na wanachama kwa uelekezi wa Zainab Abdallah. Wanahabari hupamba gwaride la shule kwa taarifa kemkem za matukio ya wiki kila Ijumaa wakiongozwa na Floyd Ogola almaarufu ‘Bingwa Mpenda Soka’, Daudi mwana wa Stefano na Desma Achieng.

Kitengo cha Uandishi huchangia maandalizi ya miongozo ya vitabu teule vya fasihi vinavyotahiniwa katika KCSE. Zaidi ya kushughulikia baadhi ya mada zinazowatatiza madarasani, wanachama hutumia vikao vyao pia kuzamia uandishi wa insha katika ‘Taifa Leo’.

Kila mwisho wa mwaka, chama huandaa dhifa ambayo pia hutoa fursa kwa wanachama wa kidato cha nne kukabidhiwa vyeti vya uanachama. Chama kinapania pia kuchapisha jarida la Kiswahili kila mwaka.

Kubwa zaidi katika maazimio ya CHAKIKA ni kuweka wazi umuhimu wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, kustawisha makuzi ya lugha, kuwapa wanafunzi jukwaa maridhawa la kuzamia uandishi wa kazi bunilizi, kuboresha matokeo ya KCSE na kuzidisha maarifa ya utafiti katika uanahabari na fani nyinginezo zinazofungamana na Kiswahili.

  • Tags

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Ulinganifu wa hali hasi katika methali za...

USHAURI NASAHA: Yajaze mazingira yako uchangamfu ili ufuzu...

T L