• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
USHAURI NASAHA: Yajaze mazingira yako uchangamfu ili ufuzu vyema zaidi

USHAURI NASAHA: Yajaze mazingira yako uchangamfu ili ufuzu vyema zaidi

NA HENRY MOKUA

JE mazingira yako ya kufanyia kazi, ya kusomea huwaje?

Je waweza kuwa kiini cha uchangamfu kwa wenzio?

Je wewe mwenyewe huweza kuchangamka kiasi cha kuyafanya mazingira yako kuvutia?

Tunaishi katika enzi ambapo uchekeshaji ni kazi ambayo hulipiwa vizuri tu na huwafaidi wengi – wachekeshaji wenyewe pamoja na hadhira zao.

Hivi ni kwa sababu uchangamfu una manufaa kadha kiafya na kiakademia! Je uchangamfu una manufaa gani katika muktadha wa shuleni – hasa miongoni mwa wanafunzi.

Uchangamfu ni msingi muhimu wa ubunifu. Unapokuwa na hasira, unaelekea kukata tamaa kuhusiana na mengi. Aghalabu unaukosa mwamko wa kuyafanya hata mambo ya msingi yanayokujuzu kwa kuona kwamba hayana faida kwako tena. Uchangamfu na furaha lakini ni dawa muhimu kwa changamoto hii kwani hukuchochea kufikiri kwa mapana na kwa kina kirefu. Katika harakati ya kufikiri huku, kuna uwezekano mkubwa waweza kuvumbua jambo fulani likawa la msaada mkubwa kwako na kwa wenzio.

Mtazamo chanya ambao ni muhimu sana kwa mwanafunzi huchangiwa mno na uchangamfu. Unapoukosa uchangamfu unakuwa katika hatari kubwa ya kuugemea mtazamo hasi ambao utakufanya kuyaona maisha kama magumu sana hata ambapo una nafuu ya mambo mengi.

Mtazamo chanya kwa upande wake huyafanya hata mambo yanayoonekana magumu yakawa mepesi. Hivi ni kwa sababu unaweza kuwazia mibadala mingi ya kuyashughulikia. Aidha waweza kuanza kwa asilimia ndogo na kadri unavyokuwa na uzoefu unaweza kuyafanya kikamilifu.

Hebu na iwe hiari yako kuyabuni mazingira yaliyojaa uchangamfu au kuuchangia uliobuniwa na wengine ili kuzua mazingira yenye utulivu na yanayoweza kufanikisha shughuli zako na za wenzio.

  • Tags

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Kayole...

NGUVU ZA HOJA: Ikiwa Sheng ni kizawa cha Kiswahili,...

T L