• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wahudumu wa bodaboda watadhibitiwa kupitia miungano ya ushirika – Sacco

Wahudumu wa bodaboda watadhibitiwa kupitia miungano ya ushirika – Sacco

Na SAMMY WAWERU

TUKIO la mwanadada kuonekana akidhulumiwa na wahuni wanaoshukiwa kuwa wahudumu wa bodaboda kufuatia kanda ya video iliyosambazwa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii, ni hujuma na unyama usiomithilika.

Haki za kibinadamu na za kimsingi za msichana huyo mwanadiplomasia raia wa Zimbabwe, zilikiukwa. Tukio hilo la kikatili na ambalo limekashifiwa vikali, lilitekelezwa katika barabara ya Prof. Wangari Maathai, jijini Nairobi.

Linasemekana kufanyika mnamo Machi 4, japo lilifichuka mapema wiki iliyopita. Washukiwa 16 walitiwa nguvuni na pikipiki zao kutwaliwa. Walifikishwa mahakamani na wanaendelea kuzuiliwa, uchunguzi uliendelea.

Mshukiwa mkuu wa kitendo hicho, Zachariah Nyaora Obadia, aliyekuwa mbioni baada ya kutambuliwa, alikamatwa Jumatatu na makachero wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Uhalifu (DCI).

Kulingana na DCI, alitiwa nguvuni eneo la Isebania boda ya Kenya – Tanzania akiwa katika harakati za kutorokea nchi jirani. Kamatakamata ya wahudumu wa bodaboda kote nchini, jana ilisimamishwa mnamo Jumamosi, ilitekelezwa saa chache baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kukashifu tukio hilo na kuagiza uchunguzi kuanzishwa mara moja.

“Lazima tulinde barabara zetu dhidi ya matukio ya aina hiyo. Nimeamuru maafisa wa usalama kukamata wahusika na kuwachukulia hatua kisheria,” Dkt Matiang’i alisema.

Inadaiwa, mwanadada huyo alidhuhuliwa baada ya kusababisha ajali iliyohusisha mhudumu wa bodaboda. Duru zinahoji, walimpora simu na kima cha Sh130, 000 pesa taslimu.

Kulingana na Bw Wahome Thuku, wakili, hilo ni tukio la wizi wa kimabavu. “Huo ni uhalifu na wizi kupitia nguvu za kimabavu,” wakili huyo akaelezea, akiukemea vikali. Uhalifu huo ni ukumbusho jinsi sekta ya bodaboda imesheheni uozo.

Si kisa kimoja, viwili au vitatu wananchi wamekumbana navyo na kushuhudia. Ni sekta iliyosaidia kubuni mamia, maelfu na mamilioni ya nafasi za ajira miongoni mwa vijana, japo baadhi wameigeuza kuwa mtandao wa uhalifu.

Pikipiki zimeripotiwa kutumika kushiriki uhalifu, na hata mauaji ya kinyama. Tukio la msichana huyo aliyekuwa akiendesha gari, lilichochea wachangiaji mitandao kuelezea ghadhabu na hasira walivyojipata kuhangaishwa na wahudumu wa bodaboda.

“Wizi wa kimabavu ni uhalifu unaopaswa kuchukuliwa hatua kali kisheria,” Stephen Theuri akaandika kwenye Facebook, akilalamikia kisa ambapo alihangaishwa na wahudumu wa bodaboda Nairobi.

“Wafunguliwe mashtaka, na watakaopatikana na hatia kuhukumiwa kifungo cha jela,” akapendekeza @Charles Kamau, kupitia Twitter. Naye, @Jacqueline Ngure, akielezea kusikitishwa kwake na unyama huo, alisema mwanadada huyo anapaswa kupitia ushauri nasaha kwa kile alitaja kama “mkondo wake wa maisha kubadilishwa ghafla na tukio lililotishia uhai wake”.

Adhabu

Kwa mujibu wa sheria, jaribio la uhalifu linalosababisha majeraha ya mwili lina adhabu ya kifungo cha miaka 5 gerezani, wizi wa nguvu za kimabavu miaka 14, jaribio la kubaka au kunajisi zaidi ya miaka 5 na uharibifu wa mali ya kibinafsi miaka 5.

Huku wahudumu wa bodaboda wakionekana kupuuza sheria na kuzichukua mikono mwao, sekta hii inapaswa kudhibitiwa. Ndio, imeleta mchango mkubwa kiuchumi na kimaendeleo, ila mambo sasa yamezidi unga.

Sawa na sekta ya uchukuzi wa umma hasa matatu na tuktuk, inavyodhibitiwa kupitia miungano ya ushirika – Sacco, bodaboda zinapaswa kupitia mkondo huo. “Pikipiki zote zilizoko katika usafiri na uchukuzi wa umma, ziandikishwe kupitia Sacco. Itakuwa rahisi kudhibiti wahudumu,” ashauri King’ori Wa Mugure.

Kulingana na Bw King’ori, miungano ya ushirika itasaidia kwa kiasi kikubwa kulainisha sekta hiyo. Hofu ikiibuka huenda baadhi ya wale ambao hawakushiriki kudhulumu msichana huyo wakajipata kwenye kikaangio moto, kwa kuwa katika eneo la kisa, Sacco itasaidia kutambua upesi wanaoshiriki uhalifu.

You can share this post!

Urithi wa Joho wazua taharuki

Nzoia Sugar wajiondoa kutoka mduara wa kushushwa ngazi

T L