• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 3:55 PM
Urithi wa Joho wazua taharuki

Urithi wa Joho wazua taharuki

WACHIRA MWANGI NA WINNIE ATIENO

WANASIASA wanaotaka kuwania ugavana Mombasa kupitia Chama cha ODM, wametakiwa kutuliza uhasama wa wafuasi wao baada ya visa vya kushambuliana kuongezeka katika mikutano ya hadhara.

Viongozi wa kijamii wameonya kuwa endapo mizozano inayohusishwa na siasa za urithi wa Gavana Hassan Joho haitakomeshwa, kuna hatari ya kuathiri maisha na biashara za kaunti hiyo ambayo ni tegemeo la kiuchumi pia kwa kaunti nyingine za Pwani, taifa na nchi zinazotegemea Bandari ya Mombasa kwa biashara zao.

Wanasiasa wanaotaka tikiti ya ODM kuwania ugavana kaunti hiyo ni Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, Naibu Gavana, Dkt William Kingi, na mfanyabiashara, Bw Suleiman Shahbal.

Tukio la majuzi zaidi ambapo fujo kuhusu urithi wa kiti cha Bw Joho zilizuka lilikuwa wiki iliyopita wakati wa hafla ya kuadhimisha siku ya wanawake ulimwenguni.

Mwezi Februari, vijana wanaoaminika kuegemea pande tofauti za siasa za ugavana walishambuliana katika mkutano wa hadhara wa Azimio la Umoja uliokuwa umeandaliwa katika uwanja wa Tononoka ukiwa umehudhuriwa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.

“Tumeshtuka kwamba wafuasi wa wagombeaji wanaweza kuamua kutatiza sherehe ya wanawake. Tukumbuke kuwa wanawake wamekuwa waathiriwa wakuu wa ghasia za kisiasa kila mara. Inashangaza kuwa wanasiasa husika hawajajitolea kuwapa nidhamu wala kuonyesha uongozi bora kwa wafuasi wao wengi,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Haki Yetu, Kasisi Gabriel Dolan.

Shirika hilo lilisema endapo hatua hazitachukuliwa kuzima matukio hayo, huenda kukawa na fujo zaidi za uchaguzi kwani hata mchujo wa vyama haujafanywa ilhali huo ndio wakati fujo nyingi huanza kutokea.

Wanaharakati walitaka asasi husika ikiwemo Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kuingilia kati ili wanasiasa wanaopatikana walihusika, wachukuliwe hatua.

“Tuachane na tabia hizi mbovu na badala yake tulenge macho yetu kwa maendeleo ya wanawake. Tunatoa wito pia kwa asasi za kiusalama kuchukulia hatua waliopanga fujo hizo,” alisema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Haki Africa, Bi Salma Hemed.

Mbunge wa Jomvu, Bw Badi Twalib, alikemea fujo zilizotokea wiki iliyopita akashangaa wanasiasa wanaume walikuwa wameenda kufanya nini katika hafla hiyo.

Sherehe hizo zilikuwa zimehudhuriwa na Bw Nassir na Dkt Kingi. Ingawa Bw Shahbal hakuwepo, baadhi ya wananchi katika umati walionyesha dalili kwamba walikuwa wafuasi wake.

“Hiyo siku ilikuwa ya kusherehekea wanawake na sielewi kwa nini kulikuwa na viongozi wa kiume hapo. Wangelituma wake zao au viongozi wengine wa kike katika kaunti badala yake,” akasema Bw Twalib.

Kwa upande wake, Bw Nassir alieleza masikitiko kuhusu vurugu hizo akasema visa aina hiyo visiwahi kutokea tena.

Bw Nassir pia alionya wanasiasa dhidi ya kuendeleza siasa za chuki kwenye kinyang’anyiro cha ugavana Kaunti ya Mombasa.

“Tusidhalilishe wanawake. Silaha yetu ni kadi ya kura, na hawawezi kutupokonya. Kampeni yetu itaendeshwa kwa msingi wa matakwa ya wakazi wa Mombasa. Tuzungumze lugha ya kuunganisha wakazi wala si kuwatenganisha kwa misingi ya kisiasa,” alisisitiza.

Mbunge huyo alilaumu baadhi ya wanasiasa ambao alidai wanaendeleza siasa za chuki kwa matukio hayo ya fujo mara kwa mara.

You can share this post!

Anaswa akimfanyia babake KCSE

Wahudumu wa bodaboda watadhibitiwa kupitia miungano ya...

T L