• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Wakazi wa Juja wamlilia Wajackoyah awasaidie kukabiliana na kero la fisi wala watu

Wakazi wa Juja wamlilia Wajackoyah awasaidie kukabiliana na kero la fisi wala watu

NA MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa Juja, Kiambu sasa wanamuomba aliyekuwa mwaniaji wa urais kwa tikiti ya Roots Party, George Luchiri Wajackoyah kufika eneo hilo kuwasaidia kukabiliana na fisi ambao wamekuwa wakiwahangaisha bila huruma.

Katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, fisi hao wanasemekana kuua zaidi ya watu 20 na kujeruhi makumi ya wengine, huku serikali ikichelea kuchukua hatua ili kuwapa wenyeji afueni.

“Sasa tumeamua kama wenyeji kuchukua sheria mkononi dhidi ya fisi hawa ambao hata tunashuku sio wa kawaida. Fisi anajulikana kama mnyama muoga na ambaye ukisimama kidete unaweza hata ukamuua bila silaha yoyote. Lakini hawa fisi wa Juja ni kama mashetani wa kutumwa na nguvu za mapepo na Wajackoyah atatufaa kwa sasa,” akasema mkazi, Eustace Mbogo.

Katika hali hiyo, Bw Mbogo alisema kwamba “tumemkumbuka Bw Wajackoyah ambaye katika siasa zake za kuwania urais wa mwaka jana, 2022, alituahidi kwamba alikuwa na soko la sehemu nyeti za fisi…Tunataka sasa aje ili tukiwavamia na kuwaua, tupate riziki ya kuuza nyeti za wanyama hao”.

Baada ya fisi hao kumla mtoto wa mwanasiasa wa eneo hilo wiki mbili zilizopita katika mtaa wa Babylon, serikali iliingia katika eneo hilo na kutekeleza msako ambao uliishia katika kupigwa risasi kwa fisi wawili mnamo Desemba 1, 2023, nao wenyeji wakiua wawili siku tatu baadaye, Desemba 4.

“Lakini hilo halitoshi kwa kuwa fisi hao walijitokeza kulipiza kisasi cha wenzao kuuawa na wakamuua mwanamke mnamo Desemba 2, 2023 mwendo wa saa 11 asubuhi,” akasema Bw Mohammed Abdi, mkazi wa Juja.

Bw Abdi alitangaza kuwa tayari wenyeji wamezindua mpango unaofahamika kama “Operesheni nyorosha fisi” ambao utajumuisha wakazi wa maeneo tata kama Ndarugo, Nyacaba, Witeithie, Benver, Kigwi, Muhindi na Murigu na hata Juja Farm.

Hayo yalijiri huku mbunge wa eneo hilo Bw George Koimburi akiita mkutano wa umma katika eneo la Nyacaba Desemba 8, 2023 ili kupanga mikakati ya kukabiliana na fisi hao hatari.

Naibu Kamishna wa Juja Bw Charles Muriithi alisema kwamba “shida kubwa ni eneo hilo kuwa na vichaka na ni mashamba la watu binafsi”.

Alisema serikali inatafuta wenye mashamba hayo ili wakubali ama kuyaweka ua, waanze kuyalima ili vichaka viishe au wajenge kando na pia uwezekano wa kuyakodisha kwa wenyeji yatumike ili fisi hao wakose makao.

Hata hivyo, Bw Muriithi alisema maafisa wa idara ya Wanyamapori (KWS) pia wanafaa kumakinikia suala hilo na wawajibikie fisi hao kwa kuwa ni mali yao.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Akothee na dadake Cebbie wazika tofauti zao akimiminiwa...

Mpango wa kutuma polisi Haiti bado waendelea licha ya korti...

T L