• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Wanafunzi wanufaika na sare za shule

Wanafunzi wanufaika na sare za shule

Na MERCY KOSKEI

Zaidi ya watoto 250 kutoka familia maskini za vitongoji duni vya Rhonda na Mwariki, Kaunti ya Nakuru wamenufaika na sare za shule.

Wanafunzi hao wa shule ya Msingi ya Kibowen Komen walipata msaada huo kutoka kwa Shirika la Street Children Assistance Network Nakuru (SCANN) mnamo Jumamosi.

Kulingana na mwenyeketi wa shirika hilo, Bw Shamsher Gilani walitembelea shule hiyo na kubaini kuwa wanafunzi wengi hawana sare za shule kwa sababu ya umaskini.

Afisa huyo aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa walishauriana na mwalimu mkuu na kuchagua wanafunzi wanaotokea familia zenye kipato cha chini.

“Isitoshe, watafaidika na chakula cha mchana kwani wazazi wengi hawawezi kugharamia ada ya mlo,” alisema.

Linet Kwamboka, mzazi wa shule hiyo, alifichua kuwa amekuwa akihangaika kulea watoto wake wanne baada ya mumewe kuhukumiwa kifungo cha maisha.

Baadhi ya wanafunzi waliopata msaada wa sare. Picha / MERCY KOSKEI

Licha ya serikali kutangaza elimu ya msingi kuwa bure, Kwamboka alisema kutimiza mahitaji mengine kama vile kununua sare za watoto wake wawili bado ni changamoto.

Ili kujikimu kimaisha mama huyo anafanya vibarua kama vile kuuza samosa katika mitaa ili kukidhi mahitaji ya kimsingi ya watoto wake akisema mapato hayo ni kidogo.

“Maisha ni magumu sana hasa kama mama pekee. Watoto wangu wamekuwa wakiishi kwa neema. Msaada huu ni wa maana kwangu,” aluisema.

Naye Anastacia Kavaya, mkazi wa Rhonda na mama wa watoto wawili, alisema kuwa ana furaha kwani mwanawe mmoja aliye katika gredi ya 3 amenufaika na msaada wa sare ya shule.

Yeye ni mjane, na alisema kununua sare imekuwa changamoto kwake kwani kwa sasa ni ghali.

Shule ya Msingi ya Kibowen Komen, Nakuru. Picha / MERCY KOSKEI

Alieleza kuwa nguo inagharimu Sh700, sweta Sh 650 na viatu vikiuzwa Sh 800, mahesabu ambayo akijumuisha yanamlemea.

“Kwa sasa sijalipa kodi kwa miezi mitatu kwa sababu ya kukosa pesa. Alipokuwa anajiunga na darasa la kwanza niliweza kupata msaada kutoka kwa majirani,” alisema Bi Kavaya.

Wazazi hawa wawili ni mfano tu, masaibu yao yakiashiria taswira ya changamozo ambazo wazazi wengi katika maeneo ya mabanda hupitia ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.

Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi ya Kibowen Komen, Bw Peter Gitau alibainisha kwa masikitiko kwamba wanafunzi wengi huvaa sare za shule na viatu vilivyochanika huku wengine wakivaa nguo za nyumbani.

Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi ya Kibowen Komen Bw Peter Gitau. Picha / MERCY KOSKEI

Hili lilimsukuma Bw Gitau kulegeza sheria ya ‘kufuata sare za shule’, na badala yake kuruhusu wanafunzi ‘kuja jinsi walivyo’.

“Nilizungumza na walimu wote na kuwaambia watoto wanapaswa kuruhusiwa kuingia darasani wakiwa wamevaa nguo zozote kwa kuwa wazazi wengi hawana hata pesa za chakula,” alisema.

Hata hivyo alisema licha ya changamoto hizo, shule anayoongoza imeandikisha matokeo mazuri kwani walipata alama za wastani ya 226 – ongezeko kutoka wastani wa alama 208 ya mwaka uliopita.

“Ninahimiza serikali iendelee kutupiga jeki na pia wasamaria wema wajitokeze kusaidia shule zilizoko katika makazi ya mabanda ili kuwapa motisha wanafunzi kusoma,” Bw Gitau aliongeza

  • Tags

You can share this post!

Achinja binti na kumla

Kocha wa Kenya U20 asherehekea ‘bathidei’ kibarua cha...

T L