• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
WANGARI: Mitihani isiwe kipimo cha wanafunzi kufaulu au kufeli maishani

WANGARI: Mitihani isiwe kipimo cha wanafunzi kufaulu au kufeli maishani

Na MARY WANGARI

KWA muda sasa, tangu matokeo ya KCSE yalipotangazwa, vyombo vya habari vimekuwa vikiangazia shule zilizotia fora kwa kutoa idadi kubwa ya wanafunzi waliopata alama ya A.

Sehemu kubwa ya mahojiano na ripoti ambazo zimekuwa zikigonga vyombo vya habari imekuwa kuhusu wanafunzi waliopata alama za juu na kufuzu kujiunga na vyuo vikuu nchini.

Yote haya yamekuwa yakiendelea huku kukiwa na wanafunzi zaidi ya 60,000 ambao hawakufanikiwa kujiunga na vyuo vikuu baada ya kukosa kutimiza alama zinazohitajika.

Kama kawaida, kila matangazo ya KCSE yanapotangazwa, huwa yanaibua machozi ya furaha kwa waliopasi na machozi ya kukata tamaa kwa waliofeli.

Inasikitisha jinsi miaka minne ya maisha ya mwanafunzi huweza kufupishwa katika mtihani mmoja tu unaotarajiwa kuamua mkondo wa maisha ya mtahiniwa.

Wakati huu ambapo wanafunzi waliopasi mitihani hiyo ya kitaifa wanazidi kumiminiwa sifa tele na kusherehekewa, wenzao ambao hawakufanikiwa bila shaka wanajihisi kama wasiofaa na waliofeli maishani.

Kwa kusema hivi, lengo si kumaanisha kuwa ni vibaya kwa wanafunzi kutia bidii na kupata alama nzuri.

Kupata alama nzuri katika mtihani ni jambo la kupongezwa lakini uhalisia ni kuwa, mustakabali wa maisha ya mtu kamwe hautegemei alama alizopata.

Ni kweli alama nzuri humwezesha mwanafunzi kujiunga na chuo kikuu maarufu, na hata kupata kazi au kujunga na taaluma zinazoenziwa.

Hata hivyo, katika kizazi cha leo, alama si kigezo cha kufaulu au kutofaulu maishani katika siku za usoni.

Hali ya uchumi wa Kenya inavyoendelea, ni dhahiri kuwa itagharimu zaidi ya alama ili kufaulu maishani. Itahitaji ubunifu na ujuzi ili kujipatia riziki na kujikimu kimaisha katika kizazi hiki ambapo mifumo ya uchumi inakabiliwa na wakati mgumu.

Wakati umewadia kukoma kutumia alama katika mitihani kama kigezo cha kuwapachika wanafunzi majina ya ‘washindi’ na waliofeli.

Katika kipindi cha hivi karibuni, imezidi kubainika wazi kwamba kupata alama ‘nzuri’ au ‘mbaya’ si kigezo kinachoashiria kwamba mwanafunzi atafanikiwa au kufeli maishani katika siku za usoni.

Jinsi watu walivyotofauti, ndivyo pia walivyojaaliwa vipaji tofauti tofauti. Kuna wale waliojaaliwa kipaji cha masomo, kuna waliojaaliwa kipaji cha biashara, kilimo, spoti na kadhalika.

Sekta ya kiviwanda inaweza kunufaika mno endapo tutabadilisha mwelekeo wetu na kukubali uhalisia kuwa si watu wote waliojaaliwa katika nyanja ya elimu.

Kwa kufanya hivyo, wanafunzi wanaweza kuruhusiwa kuchagua mapema taaluma zinazoambatana na ujuzi na talanta zao na kisha kuzitilia maanani tangu mwanzo.

Hii ni kwa sababu matokeo ya mitihani ni sehemu moja tu ya safari ya maisha kwa jumla na wala si mwisho jinsi inavyosawiriwa.

[email protected]

You can share this post!

Gavana wa Wajir atimuliwa afisini

ONYANGO: BBI: Hisia za wanasiasa zadhihirisha unafiki wao