• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:42 PM
WANGARI: Utaratibu wa Waislamu kuwazika waliofariki ni mfano wa kuigwa

WANGARI: Utaratibu wa Waislamu kuwazika waliofariki ni mfano wa kuigwa

Na MARY WANGARI

MAZISHI ya marehemu mwenyekiti wa Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) na Seneta wa Garissa Mohamed Yusuf Haji hivi majuzi yalikuwa na mafunzo muhimu yanayoweza kuwafaidi wanajamii wengine.

Licha ya kuwa kiongozi maarufu aliyehudumu kwa miaka mingi katika nyadhifa kuu mbalimbali, Seneta huyo alizikwa kuambatana na sheria za dini ya Kiislamu, baada ya kuaga dunia katika Hospitali ya Aga Khan.

Kwa muda mrefu, hafla za mazishi ya viongozi na jamaa za watu maarufu nchini zimekuwa zikiandamwa na vituko vya kila aina ikiwemo kugeuzwa uwanja wa siasa chafu.

Kisa cha hivi majuzi ambapo wabunge Simba Arati na Sylvanus Osoro walilimana makonde jukwaani katika mazishi ya babake Naibu Gavana wa Kisii, Joash Maangi, ni mfano mzuri wa visanga hivyo vya kusikitisha.

Kwa wanajamii wasio Waislamu, hafla za mazishi huwaacha waliofiwa wakiwa na matatizo hata zaidi kutokana na gharama zinazowakumba katika juhudi za kuwapa buriani wapendwa wao kwa njia ya heshima.

Wakenya hasa kutoka madhehebu mengine wanaweza kujifunza mengi kutokana na utaratibu wa mazishi ya Kiislamu na kuiga mambo kadhaa muhimu.

Kwa kawaida, mazishi kuambatana na sheria za Kiislamu hufanyika katika muda wa saa 24 na katika eneo ambapo mwendazake alikumbana na mauti.

Jambo hili ni muhimu hasa wakati huu wa janga la Covid-19 ambalo lilisababisha kanuni za mazishi ya wahasiriwa wa gonjwa hilo kubuniwa.

Hali hii ya kuzingatia muda wa saa 24 kumzika mwendazake huhakikisha kwamba waliofiwa hawagharamiki zaidi kuhusiana na ada za kuhifadhi mwili kwenye mochari.

Kwa namna fulani, hii ni afueni kuu ikilinganishwa na wanajamii wasio Waislamu wanaohifadhi mwili kwa siku kadhaa huku wakiandaa maombolezi yanayowaongezea gharama hata zaidi.

Isitoshe, mazishi ya Uislamu huhusisha makaburi maalum yasiyo ghali pasipo kujali hadhi ya mwendazake katika jamii.

Aidha, ni marufuku kumzika mwendazake katika jeneza isipokuwa tu katika hali maalum ambapo kuna masharti yanayopaswa kuzingatiwa.

Jambo hili huwaondolea familia na jamaa za mwendazake mzigo wa kununua jeneza na wakati huo vilevile kuwawezesha kutimiza mapenzi ya mpendwa wao aliyeaga kwa kumzika kwa njia ya heshima.

Miongoni mwa wanajamii wasio Waislamu, hafla ya mazishi huwa ghali mno kiasi cha kufilisisha familia na jamaa waliofiwa hasa ikiwa marehemu aliacha bili ya hospitali alipokuwa akitibiwa, ambapo hulazimika kuchangisha pesa kutoka kwa wahisani.

Kisha kuna baadhi ya watu wakora wanaotumia vibaya imani na huruma ya wanajamii kuwatapeli wengine kwa kisingizio cha kuchangisha pesa za matanga.

Ni bayana kwamba wanajamii wasio Waislamu ni sharti watafakari upya kuhusu utaratibu wa mazishi.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Kalonzo, Mudavadi na Weta wajitafutie kura

Tuchel awataka Chelsea kujihadhari dhidi ya mfumaji Luis...