• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
WARUI: Changamoto tele shule zikifunguliwa leo

WARUI: Changamoto tele shule zikifunguliwa leo

Na WANTO WARUI

HUKU shule za msingi na sekondari zikifunguliwa leo kote nchini, wazazi, walimu na wasimamizi wa shule wanakabiliwa na changamoto nyingi.

Ugonjwa wa Covid-19 ambao ulisimamisha shughuli za masomo kwa muda wa miezi tisa bado haujaisha. Licha ya kuwa umeonekana ukipunguza makali yake hivi majuzi, haijulikani kama unaweza kuibua makali tena na kukatiza masomo kwa mara nyingine.

Wazazi wengi wanalalama kuwa hawana pesa za kuweza kulipia karo hasa wale wa shule za sekondari. Sare za shule na viatu vinahitajika kwani watoto wamekua katika kipindi hicho. Wengine waliacha vitabu shuleni na hawajui kama vitabu vile bado vipo.

Isitoshe kuna ununuzi wa vibarakoa vya kujinga mdomo na pua.

Uhaba wa maji ya kunawia mikono umekumba takriban kila shule. Ikiwa shule za mijini kama vile Nairobi, Mombasa na Kisumu zinatingwa na shida ya maji, sembuse za vijijini? Wizara ya Afya inapendekeza kuwepo kwa mifereji kadhaa shuleni ambayo itaweza kuwahudumia wanafunzi, walimu na wafanyakazi kila wakati. Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa shule nyingi zina chini ya mifereji mitano na hata hiyo mitano haipitishi maji.

Juzi tu Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alisema kuwa kuna wanafunzi ambao watalazimika kusomea chini ya miti kutokana na uhaba wa madarasa.

Japo alikuwa akitafuta suluhisho, ikitokea mvua inyeshe wanafunzi hao watakwenda wapi? Serikali ilikuwa imeahidi kutoa madawati shuleni lakini walimu wakuu wengi wanasema kuwa hawajapokea madawati hayo. Wanafunzi wataketi wapi au watarejelea tu hali ile ile ya kuketi sako kwa bako?

Shule nyingi zimewaajiri wafanyakazi wenye umri wa makamo. Baadhi ya walimu hasa wale wamehudumu kwa muda mrefu wana umri mkuu. Kulingana na Wizara ya Afya, hawa ndio walio katika hatari ya kuambukizwa na kuwezwa na Covid-19. Tumesikia walimu wakuu kadhaa ambao waliambukizwa maradhi haya na wakafa. Je, ni vipi serikali itaweza kulinda maisha ya wafanyakazi na walimu hawa?

Kuna wanafunzi wa madarasa ya Chekechea na Gredi ya Kwanza ambao hawawezi kukaa na barakoa kwa muda mrefu.

Wanafunzi hawa wadogo watahitaji uangalifu mkuu na maelekezo ya kutosha. Itakuwa si vyema kuwalazimisha kuvaa barakoa zile kwani wanaweza kukosa uwezo wa kupumua na kusababisha hatari zaidi.

Sheria ya kutokaribiana ni ngumu sana kutekelezwa kwa watoto.

Hata kama walimu watajaribu kuitekeleza madarasani wanafunzi wanaposoma, si rahisi kuwatenganisha wanafunzi uwanjani wanapocheza. Shule ambazo husafirisha wanafunzi kutoka nyumbani hadi shuleni na kuwarejesha jioni pia zitapata shida hii.

Leo ikiwa siku ya kurudi shuleni, tunasubiri kuona jinsi ambavyo Wizara ya Elimu itakabilina na changamoto hizi miongoni mwa nyingine nyingi.

  • Tags

You can share this post!

ODONGO: Wetang’ula atumie Matungu na Kabuchai...

Wazazi wahuzunika baada ya watoto wao kukosa fursa ya...