• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Wazazi wahuzunika baada ya watoto wao kukosa fursa ya kujiunga na Olympic Primary, Kibra

Wazazi wahuzunika baada ya watoto wao kukosa fursa ya kujiunga na Olympic Primary, Kibra

Na CHARLES WASONGA

ZAIDI ya wazazi 500 Jumatano walisongamana nje ya lango la Shule ya Msingi ya Olympic, Kibra, Nairobi, wakiwa na watoto wakiwatafutia nafasi katika hiyo skuli ambayo huandikisha matokeo mazuri katika mtihani wa kitaifa.

Hata hivyo, wazazi hao ambao wana wao walikuwa wakisomea katika shule za wamiliki binafsi zilizofungwa kutokana na janga la Covid-19, walivunjika moyo walipoambiwa kuwa nafasi hazipo.

Bw Joe Odongo, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wazazi na walimu wa shule hiyo aliwashauri wazazi hao kusaka nafasi katika shule zingine za umma katika eneo hilo kama vile Shule ya Msingi ya Ayanya, Shule ya Msingi ya Raila, Woodley Primary na Shule ya Msingi ya Kibera.

“Shule hii ya Olympic ina jumla ya wanafunzi 4,785 na madarasa 53 na hivyo haiwezi kuwasajili wanafunzi wengine wakati kama huu. Kwa hivyo, usimamizi wa shule umewashauri wazazi kujaribu bahati yao katika shule zingine za umma zilizoko katika eneobunge hili la Kibra,” Bw Odongo akawaambia wazazi hao.

Miongoni mwa wale waliofika na wana wao kusaka nafasi katika shule hiyo ni Bi Salome Nyamita Matoke mkazi wa kitongoji cha Sarang’ombe.

Bi Matoke ambaye alikuwa ameandamana na mtoto wake msichana kwa jina Deborah Matoke wa Daraja la Tatu, alisema kuwa mtoto huyo zamani alikuwa akisomea katika Shule ya mmiliki binafsi ya Nyawira, Kaunti ya Nyamira.

“Nimeamua kumleta mtoto huyu katika shule hii ya serikali kwani siwezi kumudu kulipa karo katika shule yake ya zamani ambayo hutoza Sh30,000 kila mwaka. Hii ni kwa sababu nilipoteza kazi kutokana na janga la Covid-19,” Bi Matoke akawaambia wanahabari.

Naye Mama Janet Achieng’ na mwenzake Benta Osiela walisema watoto wao walikuwa wakisomea katika shule ya Hamlet Academy, mojawapo ya shule nane zilizobomolewa wakati wa upanuzi wa eneo la reli katika mitaa wa Katwekera Julai 2020.

Awali, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alizuru shule hiyo kukagua shughuli ya kurejelewa kwa masomo baada ya masomo ya kawaida kusitishwa tangu Machi 15, 2020, kufuatia mlipuko wa Covid-19.

  • Tags

You can share this post!

WARUI: Changamoto tele shule zikifunguliwa leo

Wilson Bii aduwaza Samwel Muchai