• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Washindi wa insha za ‘Taifa Leo’ watuzwa Sh50,000 kila mmoja

Washindi wa insha za ‘Taifa Leo’ watuzwa Sh50,000 kila mmoja

NA CHRIS ADUNGO

WANAFUNZI sita walioibuka mabingwa wa kitaifa katika ‘Shindano la Uandishi wa Insha za Taifa Leo’ katika miaka ya kiakademia ya 2021 hadi 2022 walituzwa karo ya Sh50,000 kila mmoja hapo jana katika jumba la Nation Centre, Nairobi.

MwanaIddi Majaliwa wa Mtondia Highway Trinity (Tezo, Kilifi), Alvine Juma Oduor wa Lukonyi Boys (Matayos, Busia) na Rachael Ndunge Muthama wa Beauty Kid School (Kasarani, Nairobi), walitawala kitengo cha shule za msingi. Kila mmoja wao alijizolea alama 33 juu ya 40 katika Shindano Kuu la Kitaifa lililofanyika Januari 31, 2023 katika maeneo saba tofauti humu nchini – Nairobi, Mombasa, Kisumu, Kakamega, Eldoret, Nyeri na Kitui.

Queen Mwende Syengo wa St Josephine Bakhita Masinga Girls (Machakos), Abdalla Ahmed Kombo wa Lenana School (Nairobi) na Glory Wanjiru Chege wa Kahuhia Girls (Murang’a), ndio waliotia fora zaidi katika kategoria ya shule za upili.
Ahmed na Wanjiru walipata alama 14 juu ya 20 kila mmoja na kuusoma mgongo wa Mwende aliyekwangura alama 15 na kuongoza orodha ya wanafunzi wa shule za upili. Mwende ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha nne, alitawazwa mshindi wa mkumbo wa Disemba 2021 na Oktoba 2022 katika eneo la Mashariki. Ahmed, ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha tatu, aliibuka bingwa wa eneo la Nairobi katika mikumbo ya Januari na Agosti 2022 mtawalia.
Wanjiru alishinda mkumbo wa Februari 2021 katika eneo la Kati akiwa mwanafunzi wa kidato cha nne. Alikwangura alama ya ‘A’ katika KCSE Kiswahili mnamo 2021 na kupata gredi ‘A-‘. Kwa sasa anasomea shahada ya uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi (Nyeri).

Mwanafunzi Glory Wanjiru Chege wa Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Nyeri (pili kushoto) atuzwa hundi ya Sh50,000 kwa kuibuka mshindi wa mkumbo wa Februari 2021 akiwa mwanafunzi wa Kahuhia Girls, Murang’a. PICHA | CHRIS ADUNGO

Majaliwa aliandika insha bora zaidi katika eneo la Pwani mnamo Novemba 2022. Akidumisha umahiri wake katika KCPE Kiswahili, alipata alama 81 katika somo hilo na kujizolea jumla ya alama 400 zilizomfungulia lango la kuingia shule ya upili ya Asumbi Girls (Homabay) wiki hii.

Juma alishinda mkumbo wa Disemba 2021 akiwa mwanafunzi wa darasa la saba. Alikwangura alama 76 katika KCPE Kiswahili mwaka 2022 na kujizolea jumla ya alama 404 zilizompa nafasi ya kujiunga na shule ya upili ya Starehe Boys Centre (Nairobi).

Ndunge aliyeibuka mshindi wa mkumbo wa Novemba 2021 katika eneo la Nairobi, kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Alliance Girls (Kiambu).

Kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita, gazeti la Taifa Leo limekuwa likiendesha Shindano la Uandishi wa Insha miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi.

Ilikuwa hadi Mei 2016 ambapo wanafunzi wa shule za upili walianza pia kushirikishwa.

Hatua hiyo ilichochewa na haja ya kupanua wigo wa ushindani na kuhimiza zaidi makuzi ya Kiswahili kupitia mradi wa usomaji magazeti shuleni (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Mhariri Msimamizi wa Taifa Leo, Bw Gilbert Mogire, alitumia hafla ya jana Alhamisi ya kutuzwa kwa washindi sita bora wa kitaifa kuhimiza wanafunzi na walimu kuthamini lugha ya Kiswahili ambayo sasa ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi.

“Taifa Leo ni hazina kubwa ya elimu. Wekeni Kiswahili mahali pake na zidini kutambua vipaji vyenu. Tuna mipango ya kupanua wigo wa shindano hili katika muda wa miezi mitano ijayo na kufadhili idadi kubwa zaidi ya wanafunzi,” akasema Bw Mogire.

Bw Stephen Musamali, ambaye ni mhariri mwandamizi wa Masuala ya Elimu katika Taifa Leo, alisisitiza kuwa uandishi wa insha ndio msingi wa taaluma ya uanahabari na hata utunzi wa hadithi fupi, novela, tamthilia na riwaya.

Kuanzia mwanzo hadi mwisho wa kila mwezi, mada huchapishwa gazetini kwa wanafunzi kuandika insha za mikumbo mbalimbali.

Kwa manufaa ya shindano, nchi imegawanywa katika maeneo saba – Nairobi, Nyanza, Magharibi, Pwani, Kaskazini Mashariki/Mashariki, Kati na Bonde la Ufa. Jumla ya washindi 14 hupatikana kila mwezi; yaani saba kutoka shule za msingi na saba kutoka shule za upili.

Wanafunzi wanaoibuka washindi kila mkumbo hujizolea Sh4,000 kila mmoja, walimu wao Sh4,000 na shule pia hutuzwa Sh4,000.

Mhariri wa Taifa Leo, Bw Ali Shisia, alisema washindi wa shindano hilo watakuwa na mchango mkubwa sana katika makuzi ya Kiswahili ndani na nje ya shule zao.

“Sisi pia tulianzia mahali fulani. Ushindi wa aina hii ni kiamsha hamu kwa wanafunzi hawa kuanza kutambua ukubwa wa uwezo wao katika Kiswahili,” alisema katika kauli iliyotiliwa mkazo na mshirikishi wa mradi wa NiE, Bw Danstone Bobea.

“Fedha hizi kutoka Taifa Leo zimewapunguzia wazazi gharama ya kuhangaikia karo kadri ninavyojiandaa kujiunga na Asumbi Girls. Nitazidi kuwa msomaji wa gazeti hili hata katika shule ya upili,” akasema Majaliwa.

“Umahiri wa kujieleza kupitia maandishi ni upekee niliojipatia kutokana na kusoma Taifa Leo. Sitaacha kuwa balozi halisi wa Kiswahili,” akaongeza Wanjiru.

Taifa Leo ni chapisho ambalo linazidi kuwachochea wanafunzi wetu kutia fora katika somo la Kiswahili. Kupitia magazeti haya, wanafunzi wamejiweka katika ulazima wa kufahamu lugha, jambo ambalo ni la msingi mno katika uelewa wa masomo mengine,” akasisitiza mwalimu David Wachira Ndegwa wa Starehe Boys Centre & School.

  • Tags

You can share this post!

Raia 8 wafariki katika zogo na kikosi cha UN

KASHESHE: Rapa Wakazi amtoa rangi Babu Tale

T L