• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
WASONGA: Serikali itenge fedha kununua dozi zaidi za chanjo ya corona

WASONGA: Serikali itenge fedha kununua dozi zaidi za chanjo ya corona

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Kusambaza Chanjo ya Covid-19 kwa Mataifa Maskini (Covax) mnamo Ijumaa lilitangaza kuwa, Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo mgao wao wa dozi za chanjo hiyo ulipunguzwa baada ya mataifa mengine kujumuishwa kwenye orodha.

Kenya sasa itapokea dozi 3.5 milioni katika awamu tofauti, badala ya 4.1 milioni zilizopangiwa awali.

Hii ina maana kuwa Kenya italazimika kujinunulia chanjo zaidi ili iweze kutimiza lengo lake; la kutoa kinga hiyo kwa angalau wananchi 17 milioni ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2021.

Idadi hii ni sawa na asilimia 30 ya Wakenya milioni 47 walio nchini.

Wataalamu wanasema iwapo Kenya itafanikiwa kutoa chanjo kwa kiwango hicho cha wananchi, itafaulu kupunguza maambukizi ya virusi vya corona, ambavyo husababisha ugonjwa wa Covid-19, kwa kiasi kikubwa sababu watu hao watapata kinga mwilini.

Lakini kinaya ni kwamba serikali haijatenga fedha mahususi kufadhili mpango wa ununuzi na usambazaji wa chanjo ya Covid-19 katika Taarifa ya Sera kuhusu Bajeti (Budget Policy Statement) ya mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai, 2021.

Ilitarajiwa kuwa Wizara ya Afya ingetenga Sh4.5 bilioni kwa ajili ya mpango huo, licha ya kwamba Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo yameorodheshwa na Covax kupewa chanjo bila malipo.

Kwa hivyo, naunga mkono wito wa wabunge na maseneta kwamba Wizara ya Fedha itenge pesa za kutekeleza mpango huo wakati wa kutayarisha makadirio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022.

Ilikuwa kosa kubwa kwa maafisa wizara hiyo ya fedha kutotaja suala hilo katika taarifa ya sera iliyowasilishwa katika Bunge na Seneti kwa uchambuzi.

Huenda maafisa fulani wa wizara walifanya hivyo kimakusudi ili fedha za mpango huo wa kupambana na janga la corona zifichwe chini ya Wizara ya Afya, na hivyo kutoa fursa yazo kuporwa na kufujwa.

Mwaka 2020 tuliona namna fedha zilitolewa na mashirika ya ufadhili, kama vile Benki ya Dunia (WB), zilifujwa na kuibiwa kwa sababu ziliwekwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya.

Kwenye ripoti iliyowasilishwa bungeni kuhusu matumizi ya Sh1.5 bilioni zilizotoka kwa WB, ilibainika kuwa jumla ya Sh4.4 milioni zilitumika kuwanunulia wahudumu wa afya chai na mandazi pekee kwa mwezi mmoja!

Wizara ya Fedha inafaa kutenga fedha mahususi za mpango mzima wa kununua na kusambaza chanjo.

Hiyo itawezesha Bunge na asasi nyingine za kukagua matumizi ya fedha za umma, kufuatilia jinsi fedha hizo zinavyotumiwa.

Serikali ikome kutegemea chanjo ya bwerere kutoka kwa COVAX, msaada ambao tayari unategemewa na mataifa mengi maskini kote ulimwenguni.

Iweke mikakati ya kununua chanjo kwingineko na kujazilia dozi zile za kutoka kwa shirika hilo, ili ifaulu katika kampeni yake ya kudhibiti msambao wa corona.

You can share this post!

TAHARIRI: Handisheki bila amani haitoshi

NGILA: Wanawake barani Afrika wachangamkie teknolojia