• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 10:59 AM
Watengenezaji malisho ya mifugo waomba muda kuongezwa kuagiza kutoka nje malighafi yasiyotozwa ushuru

Watengenezaji malisho ya mifugo waomba muda kuongezwa kuagiza kutoka nje malighafi yasiyotozwa ushuru

NA SAMMY WAWERU

WASAGAJI chakula cha mifugo wameisihi serikali kurefusha Notisi ya Gazeti Rasmi la Serikali inayowaruhusu kuagiza nje malighafi yasiyotozwa ushuru.

Kupitia Muungano wa Viwanda vya Kutengeneza Malisho ya Mifugo Nchini (Akefema), wametaka waongezewe muda wa miaka mitatu zaidi.

Hali kadhalika, wameililia serikali kuondoa ushuru unaotozwa malighafi ya chakula cha mifugo wakihoji hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama ya juu inayohangaisha wafugaji.

Notisi hiyo ya Desemba 2021, ilichapishwa kuruhusu viwanda vilivyosajiliwa kuagiza nje ya Kenya malighafi yasiyo na bidhaa za GMO ili kuunda malisho ya mifugo.

Muda wake ulikamilika mwezi uliopita, Oktoba, na kulingana na Akefema kurejeshwa kwa ushuru kutaumiza wafugaji.

Bei ya chakula cha mifugo imeandikisha kuongezeka kwa kiwango cha juu hasa janga la Covid lilipotua nchini.

“Tunapozungumza hivi sasa, hali ni mbaya zaidi kuliko mwaka uliopita. Bei ya mahindi na malighafi masoko ya kimataifa imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40,” akasema Bw Martin Kinoti, Katibu Mkuu Muungano huo kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Kikao hicho kiliandaliwa na Akefema kwa ushirikiano na Shirika linalohamasisha Matumizi ya Bayoteknolojia kwenye Kilimo (OFAB-Kenya).

Akisikitikia gharama ya juu kutengeneza chakula, afisa huyo alisema imechangia zaidi ya viwanda 40 kufungwa.

Kando na ombi la ushuru, wafugaji wanahimiza serikali kuzindua mpango wa ruzuku ya chakula cha mifigo.

“Utatuletea afueni kipindi hiki tunahangaika,” akasema Bi Jennifer Koome, mfugaji kutoka Meru.

Akefema na OFAB aidha walitumia jukwaa hilo kutoa msimamo wao kuhusu amri iliyotolewa na kiongozi wa nchi, Dkt William Ruto, kuondolewa kwa marufuku iliyozuia uagizaji wa malighafi na bidhaa za GMO.

Tangazo la Rais Ruto limeruhusu ukuzaji wa mimea iliyoboreshwa kwa jeni – GMO, na kuidhinishwa na taasisi husika za kilimo na utafiti.

Amri hiyo iliwekwa mwaka wa 2012.

Mashirika hayo yamesifia tangazo la Dkt Ruto, yakisema yanaenda sambamba na kampeni yao kuondolewa kwa makataa hayo.

Kinoti alisema hatua kuruhusu uagizaji bidhaa za GMO, ni mojawapo ya mikakati kupunguza gharama ya juu ya chakula cha mifugo.

“Tuna imani na Mamlaka ya Kitaifa Kuangazia Usalama wa Viumbe kudhibiti bidhaa zinazoingia nchini,” akasisitiza.

Kauli tofauti zimetolewa kuhusu GMO, baadhi ya viongozi na wanasiasa wakikosoa tangazo la rais.

Mwenyekiti OFAB-Kenya ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu International Service for Acquisition of Agri-Biotech Applications (ISAAA), Margaret Karembu ameutaka umma kutofautisha kati ya ukweli na hekaya akisema wanaopinga GMO “wamekosa ufahamu mimea iliyoboreshwa inavyotafitiwa na kuidhinishwa”.

Dkt Margaret Karembu, Mwenyekiti OFAB-Kenya. PICHA | SAMMY WAWERU

Dkt Karembu alisema mimea na bidhaa za GMO imekuzwa, kuuzwa na kuliwa kwa muda wa miaka 25 mfululizo, akishangaa ni kwa namna gani wanaokosoa wanakwepa kutathmini hilo.

“Mataifa yaliyokumbatia mifumo na vumbuzi za bayoteknolojia kuzalisha chakula, yameweza kuangazia kero ya chakula na njaa,” akafafanua.

“Wanaosafiri ng’ambo wamekuwa wakila chakula cha GMO, pamoja na familia zao.”

Ulimwenguni, nchi 29 zimeidhinisha kilimo cha mimea ya GMO 19 zikiwa zilizoimarika kimaendeleo.

Muungano wa Viwanda vya Kutengeneza Malisho ya Mifugo Nchini (Akefema) na Shirika linalohamasisha Matumizi ya Bayoteknolojia kwenye Kilimo (OFAB-Kenya), wasifia kuondolewa kwa amri kuzuia uagizaji bidhaa za GMO. PICHA | SAMMY WAWERU
  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Wanasiasa Nyanza wanaosaka kazi serikalini...

Vidokezo vya maandalizi ya chakula kwa wenye shughuli nyingi

T L