• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:50 AM
ZARAA: Jinsi miwa inavyotumika kuunda bidhaa tofauti

ZARAA: Jinsi miwa inavyotumika kuunda bidhaa tofauti

NA SAMMY WAWERU

MWAKA wa 2017 Kenya ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya karatasi za plastiki.

Miaka mitano baadaye, amri hiyo inaonekena kulegea kutekelezwa kwani baadhi ya wafanyabiashara wanaendelea kuuza mifuko hiyo.

Shabaha ikiwa kulinda mazingira, bidhaa hiyo haramu imeyaathiri kwa kiwango kikuu. Mosi, zinapotupwa na kutapakaa zinaharibu udongo kutokana na kemikali zinazotumika kuziunda, sekta ya kilimo ikiathirika moja kwa moja.

Hata hivyo, mashirika na kampuni tofauti zimekuwa zikijaribu kuweka mikakati ya kulinda mazingira.

Katika harakati hizo, zimejipata pia zikibuni bidhaa za aina yake pamoja na nafasi za ajira katika maeneo zinakoendeshea shughuli zake.

Kampuni ya Kibos Distillers Ltd ni mojawapo ya kampuni ambazo zinaendelea kuvumbua bidhaa tofauti zinazoweza kuundwa kutokana na zao la miwa mbali na inayotambuliwa zaidi ya sukari.Kampuni hiyo hutumia maganda ya miwa kuunda bidhaa tofauti.

“Tunayageuza kuwa karatasi mbalimbali, zinazotumika kuunda maboksi ya kupakia bidhaa,” akasema Saima Juneja, mwakilishi wa Idara ya Mauzo na Ununuzi katika kampuni hiyo.

Wao pia huuzia kampuni zinazotengeneza mifuko au hata maboksi karatasi walizounda kutokana na miwa.

“Kimsingi, ni malighafi salama kwa mazingira,” afisa huyo anaelezea, akisisitiza kwamba ubunifu huo ni miongoni mwa mikakati ya kampuni ya Kibos kudumisha mazingira.

Isitoshe, maganda ya miwa almaarufu bagasse wanayatumia kutengeneza sahani.

Saima Juneja akionyesha sahani zilizotengenezwa kwa maganda ya miwa. PICHA | SAMMY WAWERU

Si hayo tu, viwanda vya kampuni hiyo vilivyoko chini ya muungano wa Chatthe Group, kwa kutumia molasi (masalia baada ya kupata sukari), vinaunda mseto wa malighafi kama mafuta ya stovu za kisasa na sanitaiza.

“Hivi karibuni tutazindua kiwanda cha mboleaasilia,” Juneja akaambia Akilimali , wakati wa maonyesho ya Propaper yaliyofanyika jijini Nairobi majuzi.

Maonyesho hayo pia yalishuhudia kampuni nyingine kama Yashtech, kutoka Dubai, inayounda pia baadhi ya bidhaa zake kwa kutumia maganda ya miwa.

Meneja wa Mauzo, Sreerag Remesh akikadiria sahani hizo hugharimu kati ya Sh15 – 30, alisema hutumika kupashia mlo moto kwa kutumia kikangazi (microwave).

“Tukumbatie matumizi ya sahani na bidhaa za kula zisizoharibu mazingira,” akahimiza.

“Plastiki zinapozikwa udongoni, zinachukua mamilioni ya miaka kuoza.”

Naye Sanjeev Singhai, Mkurugenzi Shree Krishna Paper Mills and Industries Ltd kutoka India alitoa jawabu la kero ya matumizi ya mifuko ya karatasi za plastiki Kenya.

Alidokeza kwamba kampuni yake hutengeneza mifuko ya khaki, kwa kutumia magazeti, katoni na vitabu vilivyotupwa. Hali kadhalika, huunda mabahasha.

“Baada ya bidhaa kutumika, tunazichakata (recycle,” akasema.

Shirika lake lina soko tayari Amerika, Uingereza na katika mataifa ya Uarabuni (UAE). Ni uvumbuzi na bunifu ambazo zikikumbatiwa nchini, mbali na kuokoa mazingira zitawapa wakulima hasa wa miwa mianya mbadala kujipa mapato.

  • Tags

You can share this post!

Mshukiwa wa ulaghai akana kuwapunja wauzaji magari Sh3...

10 wafariki, 5 walazwa baada mkasa wa moto

T L