• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
10 wafariki, 5 walazwa baada mkasa wa moto

10 wafariki, 5 walazwa baada mkasa wa moto

NA KITSEPILE NYATHI

BULAWAYO, ZIMBABWE

WATU kumi waliaga dunia kwa kuteketea katika mkasa wa moto huku wengine watano wakitibiwa hospitalini baada ya kuvuta moshi.

Polisi walisema kisa hicho kilitokea mnamo Jumatatu katika shamba moja kusini mwa Zimbabwe.

Aidha, ripoti zasema polisi waliitwa kwenye shamba la Esigodini lililoko kilomita 40 kusini mwa mji wa pili mkuu wa Bulawayo.

Zaidi ya hayo ni kwamba, polisi walisema walipokea ripoti ya kisa hicho mchana baada ya taarifa kwamba, watu kadhaa walikufa kutokana na moto huo uliokuwa mkubwa.

Baada ya moshi mwingi uliofuka kwenye eneo la tukio kutulia, maafisa wa polisi walipata miili 10 ya wafanyakazi wengi wa shambani huku baadhi yao wakiwa wameteketea kiasi cha kutotambulika.

Kisa hicho kilithibitishwa na Afisa wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira (EMA) Descent Ndlovu.

“Nimepokea habari kamili kutoka kwa watu wetu kwamba, kuna watu ambao wamefariki baada ya kuteketea motoni. Ninasikitishwa na kisa hicho. Ninachojua ni kwamba, kuna vifo 10,” Bw Ndlovu alisema.

Baadhi ya walioshuhudia walisema mmiliki wa shamba hilo aliomba msaada wa wafanyakazi wake na wengine kuzima moto huo uliochochewa na upepo mkali.

“Tulikuwa tukipambana kuuzima moto huo tukiwa watu kadhaa na kwa bahati mbaya tulizingirwa na miale ya moto huo mkali uliofunika eneo kubwa. Kulikuwa na upepo mkali ambao ulisukuma moto kuelekea upande wetu,” Bw Mhlaliswa Ngwenya, mmoja wa walionusurika akasema.

Bw Ngwenya aliongeza kwamba, walikimbia kuelekea eneo lililoinuka lakini miale ya moto ikawazingira na ikawa vigumu kwao kutoroka.

“Tulikimbilia mlimani lakini tulizingirwa na miale ya moto na hii ilifanya iwe vigumu kutoroka,” Bw Ngwenya akasimulia.

Isitoshe, alisema alikimbia kupitia ndani ya moto huo ili aokoe maisha yake ndiposa akachomeka katika harakati hizo.

“Nilichomeka mikononi na kichwani. Nilisikia kelele za wanaume waliokuwa wakiteketezwa na moto huo. Nilianguka nilipofika kwenye barabara ya changarawe na hapo ndipo mwanaume alinisaidia na kuanza kutafuta msaada.”

Zimbabwe inapoteza karibu hekta milioni moja za misitu na nyasi kutokana na visa vya moto kila mwaka.

Vilevile, kulingana na EMA, msimu wa visa vya moto huanza mnamo Julai hadi Oktoba kwa sababu ya hali ya hewa.

Huwa kuna ukame na katika kipindi hicho hakuna mtu anayeruhusiwa kuwasha moto nje ya nyumba zao.

Kadhalika, visa vingine vya moto husababishwa na shughuli za kibinadamu ambazo ni pamoja na kilimo, uwindaji, utupaji ovyo wa vipande vya sigara, kuwasha moto kando ya barabara wakati wa kusubiri mabasi na kuwasha moto kimakusudi.

Kufuatia hali duni ya hospitali zake, majeruhi kama hao huwa na wakati mgumu kupokea matibabu yafaayo.

Hivyo basi, wengi hulazimika kuhamia hospitali za nchi jirani.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Jinsi miwa inavyotumika kuunda bidhaa tofauti

Serikali Kuu, Kaunti zashirikiana kutafuta suluhu ya...

T L