• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
ZARAA: Makadamia yalishuka bei 2020, uongezeaji thamani ukamuokoa

ZARAA: Makadamia yalishuka bei 2020, uongezeaji thamani ukamuokoa

NA SAMMY WAWERU

UGONJWA wa Covid-19 ulipotua nchini Machi 2020, Wangui Ikahu ni mmoja wa wawekezaji katika sekta ya kilimo walioathirika pakubwa.

Ni mkulima wa makadamia Kaunti ya Kirinyaga, anayeuza zao hilo ng’ambo.

Ana jumla ya ekari 18 zinazositiri zao hilo kijiji cha Kanugu, Kerugoya.

Wangui anasema marufuku ya ama kuingia au kutoka Kaunti ya Nairobi na viunga vyake, pamoja na huduma za ndege kusimamishwa kwa muda kudhibiti msambao wa virusi vya corona iliathiri biashara yake pakubwa.

Anakumbuka kisa nusura apoteze mazao ya mwaka mzima, tani tano.

“Kilo moja ya njugu za makadamia zilizokaushwa huuzwa kati ya Sh80 – 200, na bei ilishuka hadi Sh40,” asimulia, akiitaja kama ya ‘kutupa’.

Ni kutokana na hasara hiyo Wangui alishawishika kufanya mahesabu kuokoa biashara yake.

Akiwa na uzoefu wa miaka 15 kukuza makadamia, ana soko tayari nchini Italia.

“Pia, nina kandarasi na wakulima Kirinyaga, Nyeri, Meru na Embu ambapo hununua mazao yao,” adokeza.

Wangui anaambia Akilimali kwamba alifanya utafiti jinsi ya kuongeza thamani, uliojumuisha kutembelea Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Nchini (KIRDI).

Alipata mafunzo namna ya kukaanga njugu za makadamia, kuongeza thamani na kuhifadhi, huku akisaka soko bila mahangaiko wala presha.

“Tunapopokea makadamia, hupitia vipimo kadha wa kadha. Lazima yawe yaliyokomaa vyema, yasiyo na wadudu na magonjwa,” mwasisi huyo wa Kuwezesha Ltd aelezea.

Mazao ambayo hayajaafikia ubora yanapaswa kuwa chini ya asilimia 30, Wangui asema, akifafanua kwamba yanayopokewa yanaoshwa, na kukaushwa kwa jua muda wa siku 5 – 8.

Baadaye, yanaondolewa maganda na kupimwa tena kwa ratili.

“Yapo tunayopakia yakiwa mabichi, kisha mazao mengine tunayakaanga na kuweka chumvi, na bila, kupondaponda na kupakia.”

Njugu zisizowekwa chumvi, Wangui anasema zinasindikwa kuwa siagi (makamadia butter) kwa kuunga na sukari, asali, mafuta kusawazisha, na cocoa – chokoleti.

“Tunahakikisha uhalisia wa bidhaahai unasalia,” mfanyabiashara huyo asisitiza.

Ana kiwanda eneo la Sagana, na vifaa na mitambo anayotumia ni; mashine ya kukausha kwa jua, kuondoa maganda, kuoka, kupondaponda na ratili.

Wangui Ikahu (kulia) na mmoja wa wafanyakazi wake, Joy Nyanchoka wakionyesha njugu za makadamia ambazo hazijaondolewa maganda na miche ya macadamia. PICHA | SAMMY WAWERU

Njugu zilizokaangwa bila chumvi gramu 200 huuza Sh400, kipakio cha gramu 100 nacho Sh200, huku siagi kipimo cha gramu 200 akiuza Sh450.

Akiridhia mwanya huo wa uongezaji thamani alioingilia mwaka uliopita, 2021, Wangui anasema ana soko tayari la bidhaa hizo humu nchini, kuanzia Idara ya Ulinzi, maduka ya jumla, makundi ya walemavu, vilabu vya michezo, mikahawa Nairobi na Mombasa. Ni hatua alizopiga mbele licha ya kuwa na tatizo la macho, ambapo ameandikishwa kama mmoja wa wananchi wenye ulemavu (PWD).

Isaac Tongola, ni Mkurugenzi Mkuu Fairtrade Africa na anakiri mazao ya kilimo yaliyoongezwa thamani yanateka soko lenye ushindani mkuu.

“Kwa minajili ya soko endelevu, wakulima wakumbatie mifumo ya uongezaji mazao thamani,” Tongola ashauri.

Shirika hilo hutafutia wakulima soko ng’ambo, hususan wanaokuza majanichai, kahawa na maua.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Mbuzi wamemfungulia milango ya kulipa karo

IEBC yatoa mapendekezo kadhaa yanayolenga kuboresha...

T L